Wachimbamadini 41 wauawa katika mripuko mgodini Uturuki
15 Oktoba 2022Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Suleyman Soylu amesema wakati wa mripuko, watu 110 walikuwa ndani ya mgodi huo, na kwamba 58 miongoni mwao walikuwa tayari wameokolewa wakiwa salama.
''Bado moto unawaka mgodini, wachimbaji pamoja na waokoaji wamejitolea pakubwa kuhakikisha hakuna ndugu yao anayeachwa nyuma,'' amesema waziri Soylu ambaye amekwenda kwenye eneo la ajali, na kuongeza kuwa bado mchimbaji mmoja hajulikani alipo.
Soma zaidi: Wachimbaji waliookolewa baada ya siku 41
Picha za televisheni zimeonyesha makundi ya watu waliojawa na simanzi, baadhi wakibubujikwa na machozi, nje ya lango kuu la kuingia kwenye mgodi, wakisubiri kupata taarifa juu ya majaliwa ya wapendwa wao waliokuwa mgodini.
Habari za mwanzo kuhusu walionaswa mgodini zilitolewa na wenzao walioweza kukimbia haraka na kutoka nje. Meya wa wilaya ya Amsara ulipo mgodi ulioathirika, Recai Cakir amesema wengi wa walionusurika mkasa huu wamepata majeraha mabaya.
Erdogan njiani kuelekea eneo la ajali
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitarajiwa kusafiri kwa ndege kuzuru eneo la ajali hiyo, na kupitia ukurasa wake wa twitter aliapa kuwa uchunguzi wa kina utafanyika kubainisha kilichotokea.
Waziri wa nishati Fatih Donmez alidokeza baadaye kuwa kwa sehemu kubwa moto uliozuka mgodini hapo ulikuwa umedhibitiwa, huku juhudi za kupoza eneo ulipotokea moto huo, kiasi cha mita 350 chini ya ardhi, zikiendelea.
Soma zaidi: Watu 14 wafariki Congo baada ya mgodi kuporomoka
Meya wa Amsara, Recai Cakir mesema wafanyakazi wa uokozi wapatao 70 walikuwa wameweza kufika kwenye chanzo cha mripuko, katika kina cha mita zipatazo 250 chini ya ardhi.
Kulingana na waziri wa mambo ya ndani, Suleyman Soylu, wachimbamigodi 10 wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za Bartin na Istanbul, na mmoja tayari ameruhusiwa kurudi nyumbani.
Gesi ya metani ndio chanzo cha mripuko
Duru za serikali ya Uturuki zimeeleza kuwa waendeshamashtaka wameanzisha uchunguzi kujua chanzo cha moto huo. Taarifa za mwanzo hata hivyo zinaashiria kuwa gesi ya metani mgodini ndio imeuanzisha moto huo.
Soma zaidi: Wachimba mgodi 955 waliokwama Afrika Kusini waokolewa
Awali, shirikisho la huduma za kushughulikia majanga nchini Uturuki, AFAD lilikuwa limearifu kuwa moto umeanzishwa na cheche kwenye transfoma iliyokumbwa na hitilafu, lakini baadaye limeiondoa dhana hiyo, likiafikiana na ile ya mrundikano wa gesi ya metani.
Mwaka 2014, wafanyakazi 301 waliuawa katika ajali mbaya kabisa ya mgodini nchini Uturuki, katika mji wa Soma ulio umbali wa kilomita 350 kusini mwa Istanbul.
Vyanzo: rtre, afpe