1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 waudhibiti uwanja wa ndege wa Goma

20 Novemba 2012

Waasi wa M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo leo wameudhibiti uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma, baada ya mapambano makali yanayoendelea kati ya waasi na vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/16m9C
Waasi wa M23 wa Kongo

Hali hiyo imetokea wakati ambao Rwanda inavituhumu vikosi vya jeshi la Kongo vinavyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kwa kulishambulia eneo lake wakati wa mapambano na waasi karibu na eneo la mpakani hapo jana.  Msemaji wa kundi la  M23, Kanali Vianney Kazarama ameliambia shirika la habari la AP kwa njia ya simu kwamba sasa waasi wanapambana kuudhibiti mji wote wa Goma, baada ya kufanikiwa kuudhibiti uwanja wa ndege na kwamba sasa wako ndani ya mji wa Goma. Akizungumza leo na DW, Mbunge wa jimbo la Kivu Kaskazini, Mayombo Omary Bin Fikira amethibitisha kwamba waasi wameutwaa uwanja huo wa ndege. Mbunge huyo anasema kwa sasa hali ni ya kutatanisha katika mji wa Goma na milio ya risasi imekuwa ikisikika.

Rwanda haina mpango wa kulipiza kisasi

Rais Joseph Kabila na Rais Paul Kagame
Rais Joseph Kabila na Rais Paul KagamePicha: picture-alliance/dpa

Aidha, mbali na Rwanda kuishutumu Kongo, imesema haina mpango wa kulipiza kisasi kwa kile ilichokiita uchokozi unaofanywa na Kongo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa masuala ya mashariki mwa Kongo ni nyeti na hayapaswi kufanyiwa mchezo. Awali msemaji wa jeshi la Rwanda alisema jeshi la Kongo liliushambulia mji wa mpakani wa Gisenyi na kuwajeruhi watu watatu, wakati mapigano yalipokuwa yanaendelea kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 waliokuwa wakiukaribia mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini wa Goma.

Serikali ya Kongo ambayo imerudia kuishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, katika harakati zake za kudhibiti madini Kivu Kaskazini. Msemaji wa serikali ya Kongo, Lambert Mende amesema wana taarifa kuwa Rwanda imekuwa ikifyatua risasi kwenye himaya yake yenyewe ili kuhalalisha uvamizi mkubwa unaoufanya.

Umoja wa Mataifa waendelea kuishutumu Rawanda

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, shutuma ambazo zimekanushwa vikali na Rwanda. Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia anadaiwa kuwaunga mkono waasi hao amemwambia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon kwamba amezungumza na waasi kutokana na mamlaka aliyonayo kama mkuu wa eneo hilo la maziwa makuu na kutoa wito wa kuwepo utulivu. Hata hivyo, Uganda nayo imekanusha kuwaunga mkono waasi.

Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moonPicha: Getty Images

Waasi waipa serikali saa 24

Jana waasi waliipa serikali ya Kongo saa 24 kuanza mazungumzo ya amani, la sivyo itakabiliwa na mapambano mapya. Hata hivyo, serikali ya Kongo imekataa ombi hilo la waasi. Rwanda imekanusha madai kutoka kwa Kongo kwamba kiasi wanajeshi wake 4,000 wamevuka mpaka na kuingia Kongo kwa lengo la kuwasaidia waasi wa M23. Umoja wa Mataifa kwa upande wake ina wanajeshi 6,700 wa kulinda amani wa katika eneo la Kivu Kaskazini, wakiwemo 1,400 ambao wako kwenye mji wa Goma. Kutokana na mzozo huo wa mashariki mwa kongo, mawaziri wa mambo ya nje na wakuu wa usalama wanakutana leo Jumanne (20.11.2012) mjini Kampala, Uganda katika mkutano utakaoongozwa na Rais Museveni. Zaidi ya watu 500,000 wameyakimbia makaazi yao na katika kambi za wakimbizi mjini Goma, ambao unakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni moja.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman