Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wana matumaini
15 Februari 2013Matangazo
Mjumbe wa kundi la waangalizi hao, Bi. Neveka Lukin, wakati kundi la waangalizi lililo mjini Nairobi lilipotembelea vituo vya mafunzo kwa maafisa wawatakaosimamia uchaguzi mkuu kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Maafisa wa kundi hilo la waangalizi lililo mjini Nairobi wamesema kwamba kufikia sasa wameridhishwa na tathmini ambayo wameifanya siku chache baada ya kuanza kazi yao.
Akizungumza baada ya kutembelea kituo cha mafunzo kwa maafisa wa uchaguzi mkuu ujao, Bi. alisema: “Tunatumaini kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tofauti kutokana na kanuni ambazo zimewekwa zikiwemo utaratibu wa utendaji kazi kwa maafisa wa tume ya uchaguzi na waandishi wa habari kupitia baraza la vyombo vya habari nchini kuhakikishauchaguzi wa mwaka huu unakuwa tofauti na ule uliopita.”
Bi Lukin amesema kwa muda wa wiki mbili ambazo wamekuwa humu nchini, tathmini yao inaonyesha kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa amani.
“Kitu kimoja ambacho tumeona katika siku chache hizi ambazo tumekuwa humu nchini ni kwamba kila mmoja nchiniana matumaini kwamba uchaguzi mwa mwaka huu utakuwa wa amani. Wagombea wenyewe, makundi ya kijamii, watetezi wa haki za binadamu na Tume yenyewe ya uchaguzi IEBC wote wanatumani kwamba uchaguzi huu utakuwa wa amani kwani tayari mikakati na vifaa vya kutosha vya usalama kuzuia ghasia sawa na zilizotokea wakati wa uchaguzi uliopita”.
Naye Johannes Tesselaar, mmoja wa waangalizi hao anayeandamana na Bi. Nevenka, amesema kwamba shughuli ya uangalizi ni sehemu ya kuhakikisha demokrasia inazingatiwa na haipaswi kufanywa tu wakati wa uchaguzi wenyewe pekee.
“Tumetembea sehemumbali mbali katika muda wa wiki mbili zilizopita. Tumetembelea vituo kadhaa vya mafunzo kwa maafisa wa Tume ya Uchaguzi. Pia tumefanya mahojiano na makundi mbali mbali ikiwa ni pamoja na maafisa wa vyama vya kisasa waandishi wa habari na makundi ya kijamii. Tutawasilisha ripoti yetu kwa makao makuu na kujumuishwa kwenye ripoti kuu itakayotolewa siku mbili baada ya uchaguzi.”
Waangalizi hao pia wametembelea bohari la IEBC lililo na vifaa vya kufanyia uchaguzi kuhakikisha kwamba maandalizi ya uchaguzi ujao yanafanywa kikamilifu.
Ujumbe huo wa waangalizi kutoka Muungano wa Ulaya una wajumbe 18 wa muda mrefu waliowasili nchini mwishoni mwa mwezi January huku wengine 14 wakitarajiwa humu nchini tarehe 24 Februari, tayari kwa shughuli ya uchaguzi utakaofanyika tarehe 4 mwezi ujao.
Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef
Matangazo