Ujerumani haiungi mkono mgombea yeyote Kenya
15 Februari 2013Matangazo
Balozi wa Ujerumani nchini Kenya Bi Margit Hellwig-Boette ameyasema hayo kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu kuhusu amani na usuluhishaji mizozo kilichoandikwa na Prof. Johannes Michael Nebe wa Chuo Kikuu cha Trier nchini Ujerumani.
“Ni wajibu wa Wakenya kuchagua viongozi wao. Ujerumani haiungi mkono kiongozi wa ofisi yoyote. Tunaaamini kwamba Wakenya watafanya uamuzi wa busara na kuwachagua viongozi walio na sifa nzuri. Haijalishi ni nani atachaguliwa rais, ushirikiano na Mahakama ya ICC ni muhimu ili kuhakikisha haki inapatikana kwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na kujenga Kenya mpya iliyo thabiti.” Alisema Hellwig-Boette katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho.
Matamshi haya ya Balozi wa Ujerumani yanawiana na taarifa iliyotolewa wiki iliyopita na Rais wa Marekani Barack Obama kwamba uamuzi wa ni nani ataongoza Kenya umo mikononi mwa Wakenya wenyewe.
Hafla hiyo ya jana jioni ilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano Dk. Mzalendo Kibunjia, ambaye kwenye hotuba yake Dr. Kibunjia alisema:
“Tunaweza kuzika vichwa vyetu mchangani na kusema hakuna kitu kilitendeka lakinbi baada ya mrefu mambo haya yataweza kujitokeza tena na kutuandama. Badala ya kusubiri kwa muda wa miaka 40 wa mambo haya kuja kutuandama nadhani ni muhimu wakati tutakapopata serikali mpya tuweze kuanza kuzungumzia swala la maridhiano na kutafuta haki kwa wale waliopoteza maisha”.
Kitabu hicho kilichochukuwa muda wa mwaka mmoja kuandikwa ni mradi wa utafiti uliofanywa na wanafunzi 18 kutoka Chuo Kikuu cha Trier cha Ujerumani wakishirikiana na wenzao 18 kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya.
Kitabu hicho kimenakili matukio yaliyotokea wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 na kinatoa mwongozo wa jinsi ya kuepukana na taswira kama hiyo wakati wa uchaguzi mkuu mwezi ujao.
Kitabu hicho kimezinduliwa wakati ambapo mashirika ya kijamii yanafanya kampeni usiku na mchana kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa amani.
Mhariri wa kitabu hicho, Prof. Johannes Michael Nebe, anasema wakati wa kukusanya taarifa kutoka kwa waathiriwa hakupata mchango wowote kutoka kwa serikali ya Kenya.
“Hatukuweza kuona suluhisho lolote kutoka kwa serikali kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na Muungano wa Kenya Land Alliance juu ya matatizo ya ardhi ambayo ndicho chanzo cha ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi lakini tuliweza kupata ushirikiano wa mashirika ya kijamii kutoka makabila mbali mbali”.
Hata hivyo, Prof. Nebe anasema ana matumaini kwamba kitabu hicho kitatoa mafunzo kwa Wakenya na hasa vijana ambao hutumiwa kushiriki kwenye ghasia wakati wa uchaguzi na kwamba Wakenya wataweza kufanya uchaguzi wa amani huru na wa haki .
Mwandishi:Alfred Kiti/ DWNairobi
Mhariri: Mohammed Khelef
Matangazo