Vurugu zazuka Gaza baada ya shambulizi la Israel
23 Februari 2023Israel na wanamgambo wa Kipalestina wameshambuliana kwa ndege na maroketi ndani na karibu na Ukanda wa Gaza leo, siku moja baada ya shambulio baya zaidi la jeshi la Israel katika Ukingo wa Magharibi katika kipindi cha karibu miaka 20.
Soma pia: Jeshi la Israel lauwa Wapalestina 9 katika Ukingo wa Magharibi
Wizara ya Afya ya Palestina imesema Wapalestina 11 waliuawa, na zaidi ya 80 kujeruhiwa kwa risasi jana Jumatano, wakati wanajeshi wa Israel walipovamia mji wa Nablus. Jeshi la Israel lilisema lilikuwa linalenga wanamgambo wanaoshukiwa, huku afisa mkuu wa Palestina Hussein Al Sheikh akiuelezea uvamizi huo kama mauaji na kutoa wito wa ulinzi wa kimataifa kwa Wapalestina.
Kabla ya mapambazuko leo, wanamgambo wa Kipalestina walifyatua makombora sita kutoka Gaza hadi Israel, ambapo kundi la wapiganaji la Islamic Jihadi limedai kuhusika katika kujibu kile lilichokiita uhalifu mkubwa mjini Nablus. Saa mbili baadae, jeshi la Israel lilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo kadhaa ya Gaza, ikiwemo kile lilichokiita kiwanda cha silaha na kambi ya kijeshi vinavyosimamiwa na kundi la Hamas linalotawala ukanda huo.