1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen angoja hatima yake

16 Julai 2019

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen amekamilisha juhudi za za kuwania ofisi ya juu zaidi katika Umoja wa Ulaya. Akifaulu atakuwa mwanamke wa kwanza kupata nafasi ya urais wa Halmashauri Kuu ya umoja huo.

https://p.dw.com/p/3MAJm
Ursula von der Leyen | Europäisches Parlament Straßburg | Bewerbung EU-Kommissionspräsidentin
Picha: AFP/Getty Images/F. Florin

Von der Leyen, ambaye ataondoka katika wadhifa wake wa waziri wa ulinzi nchini Ujerumani, anapigiwa kura wakati huu na wanachama 747 wa bunge la Ulaya kuchukua nafasi hiyo ya rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya. Mwanamke huyo mwenye nguvu ndani ya Ujerumani amesema changamoto iliyopo kwa sasa ni namna ya kuwa na dunia iliyo na afya. Akilihutubia bunge la Ulaya akiwa mjini Strasbourg, Ufaransa, alisema angelipenda Ulaya kuwa bara la kwanza lililo na hali ya hewa ya kawaida ifikapo mwaka 2050.

Waziri Ursula von der Leyen anahitaji kura 374 kuchukua nafasi ya rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya. Hadi wakati huu anaweza tu kutegemea kura za wabunge kutoka kundi la chama cha Europeans Peoples Party ambalo ni kubwa katika bunge hilo, likiwa na viti 182. Wapo lakini wanachama wengine walioonesha uungaji mkono wao kwa Waziri Von der Leyen hii leo Jumanne.

Vyama vya mrengo wa kushoto vyampinga

Kuna wale pia wanaompinga kutoka vyama vya mrengo wa shoto vilivyo na misimamo mikali kama GUE/NGL walio na viti 41 katika bunge hilo na  wanachama wa mrengo wa kulia na unaokijumuisha chama cha Alternativ für Deutschland (AfD). Kura inayopigwa leo ni kura ya siri inayomaanisha kuwa wabunge huenda wakapiga kura kinyume na matakwa ya vyama vyao.

EU-Parlament: Ursula von der Leyen - Wahl zur Kommissionspräsidentin
Bunge la Ulaya likimpigia kura Ursula von der LeyenPicha: Imago/Z. Cheng

Hata hivyo, Ursula amepata uungaji mkono wa dakika za mwisho kutoka kwa Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk aliyemsifu kama mpambanaji wa umoja na Nguvu ya Ulaya na kusema kuwa anafaa kuchukua nafasi ya rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya.

Huku hayo yakiarifiwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anapanga kuijaza nafasi ya waziri wa ulinzi itakayowachwa wazi na Ursula Von der Leyen anayeiacha nafasi hiyo kufuatia nia yake hiyo ya kuwania urais wa Halmashauri  kuu ya Umoja wa Ulaya.

Akizungumza katika mkutano na waandishi habari mjini Berlin akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Moldovan Maia Sandu aliopo nchini kwa ziara fupi, Kansela Merkel amesema, nafasi hiyo muhimu haiwezi kubakia wazi kwa muda mrefu. Hata hivyo Kansela hakutaka jina lolote la mrithi wa Ursula Von der Leyen.

Hata hivyo kumekuwepo na fununu kwamba waziri wa Afya, Jens Spahn, ndiye anayetazamiwa kuchukua nafasi hiyo. Von der Leyen alitangaza hapo jana kuwa atajiuzulu wadhifa wake huo wa waziri wa ulinzi wa Ujerumani iwapo atashinda au la kuwa mjerumani wa kwanza kuongoza halmashauri ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

Chanzo: (dpa/afp)