Virusi vya Corona: Ulaya chini ya kifungo
Miito ya kutaka watu kujitenga na wengine na marufuku ya kusafiri imeilazimisha miji mikubwa ya barani Ulaya kusalia tupu wakati serikali kote barani humo zikichukua hatua nzito kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19
Paris chini ya kifungo
Shughuli kwenye mitaa yenye heka heka mjini Paris zimesimama kabisa baada ya Ufaransa kutangaza kuifunga nchi nzima Jumanne iliyopita. Watu hawaruhusiwi kutoka nje ya majumba ispokuwa kwa sababu za kununua chakula, kumuona daktari au kwenda kazini. Hata hivyo meya wa mji wa Paris amehimiza hatua kali zaidi wakati idadi ya maambukizi ikipanda duniani.
Ukimya kwenye mji mkuu wa Ujerumani
Siku ya Jumapili kansela Angela Merkel alitangaza marufuki kali dhidi ya matembezi nchini Ujerumani. Mpango huo wa vipengele tisa unajumuisha marufuku ya mkusanyiko unaozidi watu wawili, kuzingatia umbali wa mita1.5 baina ya watu na kuifunga mikahawa.
Wageni wapigwa marufuku, mipaka yafungwa
Pamoja na kudhibiti muingiliano wa ndani, Ujerumani imezidisha marufuku kwa wageni wanaoingia nchini humo. Kutokana na hilo, msongamano katika uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi nchini humo wa Frankfurt umepungua kwa kiwango cha chini.
Wakaazi wa Bavaria waamriwa kusalia majumbani
Wiki iliyopita jimbo la kusini la Bavaria lilitangaza kufungwa kwa jimbo zima kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona. Chini ya hatua hizo zitakazodumu angalau kwa wiki mbili, watu hawaruhusiwi kukusanyika nje wakiwa kwenye makundi na mikahawa imefungwa.
Uingereza yahimiza watu kujitenga
Uingereza imevifunga vilabu vya pombe na mikahawa kukabiliana na kuenea virusi vya corona. Waziri mkuu Boris Johanson amewatolea wito raia wote kuepuka kufanya safari zisizo za lazima na kutowasiliana kabisa na watu wengine kwa njia ya ana kwa ana kwa muda usio na kikomo.
Milan: Kitovu cha janga la Corona
Katika wiki za karibuni kitovu cha mlipuko wa vrusi vya Corona kilihama kutoka China hadi Italia. Nchi hiyo imeshuhudia ongezeko la kutisha la maambukizi na vifo. Italia imekuwa chini ya kifungo cha nchi nzima tangu Machi 10.
Vatican yafungwa
Wakati kiwango cha kutisha cha visa vya virusi vya Corona kikirikodiwa kwenye jimbo la kaskazini mwa Italia la Lambardy, miji ya Roma na Vatican imelazimika pia kusitisha mikusanyiko ya umma. Maeneo mashuhuri ya utalii kama kanisa la Mtakatifu Peter yamefungwa.
Uhispania: Moja ya mataifa yaliyoathiriwa vibaya barani Ulaya
Serikali ya Uhispania imeamua kurefusha hali ya dharura nchini humo hadi Aprili 11, kiasi mwezi mmoja tangu ilipotangazwa Machi 14. Hivi sasa Uhispania ni ya pili kwa idadi ya visa vya virusi vya corona barani Ulaya huku miji ya Barcelona na Madrid ikiwa imeathriiwa zaidi.
Kiwango cha maambukizi kinapungua Austria
Austria imeripoti ongezeko la asilimia 15 ya visa vya maambukizi ya virusi vya Corona, kiwango kidogo ikilinganishwa na asilimia 40 ya hapo kabla. Matokeo hayo yamepatikana baada ya serikali kutangaza hatua pana za watu kujitenga kote nchini humo. Hata hivyo mamlaka mjini Vienna zinalenga kupunguza maambukizi hadi chini ya dijiti moja katika kipindi cha wiki tatu zinazokuja.