1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wakuu wa Libya wakubaliana kuunda serikali mpya

11 Machi 2024

Viongozi watatu wakuu nchini Libya wamekubaliana juu ya umuhimu wa kuunda serikali mpya ya umoja ambayo itaratibu uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/4dNRQ
Mohamed al-Menfi na Khalifa Haftar
Mkuu wa Baraza la Rais, Mohamed al-Menfi (kushoto) na mbabe wa kivita Khalifa Haftar.Picha: twitter.com/Mohamedelmonfy

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Baraza la Rais, Mohamed Menfi, Mwenyekiti wa Baraza Kuu, Mohamed Takala, ambao wote wako mjini Tripoli, pamoja na Spika wa Bunge, Aguila Saleh. 

Katika taarifa ya pamoja, viongozi wote watatu wametoa wito kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya na jumuiya ya kimataifa kuunga mkono mapendekezo yao.

Soma zaidi:  Uchaguzi wa rais nchini Libya uko mashakani

Miongoni mwa mapendekezo yao ni makubaliano ya kuundwa kwa kamati ya kiufundi itakayotizama vipengele vilivyo na utata.

Viongozi hao walikutana mjini Kairo nchini Misri, kwa mwaliko wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit.

Mchakato wa kisiasa wa kutatua mzozo wa zaidi ya muongo mmoja nchini Libya umekwama tangu uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba 2021 kushindwa, huku kukiwa na mizozo kuhusu wagombea wakuu wanaostahiki kuwania uchaguzi huo.