Nigeria,Libya na Afrika-bara la Matumaini-Magazetini
13 Juni 2014Tuanzie na Nigeria ambako serikali ya rais Goodluck Jonathan inazongwa na matatizo ya kila aina:Baada ya visa vya kigaidi vya Boko Haram,Jonathan anakabwa na mtihani mwengine,nao ni ule wa aliyekuwa mkuu wa benki kuu ya Nigeria,Sanusi Lamido Sanusi kugeuka kuwa Amiri,au kiongozi wa mji mkubwa wenye wakaazi wengi zaidi wa kiislamu nchini Nigeria-KANO.Die Tageszeitung linaandika kuchaguliwa Sanusi kuwa Amiri wa Kano ni changamoto kwa Jonathan.Baada ya kusifu mchango wake katika kuurekebisha mfumo wa benki nchini Nigeria,Die Tageszeitung limelinukuu jarida la kimarekani la Time Magazine lililomtaja mwanauchumi huyo mwenye umri wa miaka 52 kuwa miongoni mwa watu mia moja wenye ushawishi mkubwa zaidi ulimwenguni.Hata hivyo shauku kuhusu madaraka mepya ya Sanusi si kubwa hivyo.Baada ya kutangazwa amiri tu,mamia ya vijana waliandamana mjini Kano kupinga uamuzi huo.Wangependelea zaidi kumuona Sanusi Ado Bayero,mtoto wa kwanza wa kiume akimrithi babaake aliyefariki ijumaa iliyopita.Maoni hayo linaandika die Tageszeitung yanaungwa mkono pia na rais Jonathan aliyempokonya Sanusi Lamido Sanusi wadhifa wa kiongozi wa benki kuu,mwezi february uliopita ,baada ya miaka minne tu madarakani.Gazeti hilo la mji mkuu linakumbusha jinsi mwanauchumi huyo alivyokuwa akikosoa uzembe wa serikali katika kupambana na rushwa pamoja na madai kwamba kampuni ya mafuta ya taifa NNPC imetumia vibaya dala bilioni 20 za umma.Ni nadra kwa lawama kali kama hizo kutolewa hadharani nchini Nigeria linaandika die Tageszeitung.Kurejea madarakani kama mtemi ni pigo kwa rais Jonathan linamaliza kuandika die Tageszeitung linalofafanua umuhimu wa amiri wa Kano na mfalme wa Sokoto katika harakati za kisiasa nchini Nigeria.
Juhudi za kuleta demokrasia Libya
Vurugu nchini Libya pia zimemulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii.Lilikuwa gazeti la Frankfurter Allgemeine lililoandika kuhusu kisa cha kulazimishwa na korti ya katiba ajiuzulu waziri mkuu Ahmad Maitig.Angalao kwa sasa vurugu za kisiasa zitapungua,linaandika Frankfurter Allgemeine.Vyombo vya habari mjini Tripoli,linasema gazeti hilo mashuhuri la Ujerumani,vimesherehekea uamuzi huo kuwa ni "wa kihistoria katika kuijenga Libya ya kidemokrasia.Juhudi za kuimarisha mfumo wa demokrasia zitapata nguvu uchaguzi wa bunge utakapoitishwa wiki mbili kutoka sasa linamaliza kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine.
Afrika Bara la Matumaini
Mada ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inaturejesha hapa hapa Ujerumani ambako gazeti la der Tagesspiegel linajiuliza kwanini makampuni ya Ujerumani yanabaki nyuma barani Afrika licha ya neema kubwa iliyoko barani huo?Vita,maradhi,rushwa;hiyo ndiyo picha iliyoganda vichwani wa wajasiria mali wengi wa Ujerumani wanapofikiria kuhusu bara la Afrika.Picha hiyo mbaya pengine ndio sababu kwanini biashara ya nje ya makampuni ya Ujerumani kwa bara la Afrika imetuwama katika mstari wa asili mia 2.3 na kwamba makampuni 100 yanayoendesha shughuli zake kwa sasa barani humo hayawakilishwi ipasavyo.Der Tagesspiegel linawanukuu wataalam wa kiuchumi wakisema bara la Afrika sio tu lina neema ya mali ghafi bali pia huko ndiko yatakakoibuka maeneo ya uzalishaji na soko la siku za mbele.Hadi mwaka 2020,wachunguzi wa masuala ya kiuchumi wanatarajia tabaka ya kati itaongezeka barani Afrika na kwa namna hiyo kuinua idadi ya wanunuzi.Uchunguzi uliofanywa na kuwahusisha wataalam wa kiuchumi na mameneja kutoka makampuni 15 ya magari,teknolojia ya habari na mawasiliano sawa na uhandisi umebainisha wanamkakati wanaliangalia bara la Afrika kuwa ni bara la matumaini ya ukuaji wa kiuchumi ambako makampuni ya Ujerumani yanaweza pia kufaidika-
Hadi wakati mwengine katika ukurasa kama huu,ni Oummilkheir ninaekushurukuni na kukuageni kwakherini.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Basis/Presser/All/presse
Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman