1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia waunga mkono uhuru wa Ukraine

17 Juni 2024

Viongozi wa dunia wameunga mkono Uhuru wa Ukraine na umuhimu wa kufanyika mazungumzo na Urusi ya namna ya kumaliza vita kati ya mataifa hayo. Lakini viongozi hao hawakuweka wazi lini mazungumzo hayo yatakapofanyika.

https://p.dw.com/p/4h8Ru
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Picha: EPA/MICHAEL BUHOLZER

Baada ya zaidi ya miaka miwili ya uvamizi wa Urusi Ukraine, viongozi na maafisa wakuu wa zaidi ya mataifa 90 walikusanyika katika eneo la mapumziko la Bürgenstock nchini Uswisi kwa mkutano wa siku mbili wakijaribu kutatua mgogoro huo mkubwa kutokea barani Ulaya tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia. 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisifia mafanikio ya kidiplomasia ya mkutano huo ambao Urusi haikualikwa.

Soma pia:Viongozi wa dunia waunga mkono suluhisho la amani kwa mzozo wa Ukraine

Zelesnky amesema Urusi inaweza kuwa na mazungumzo na Kiev hata kesho iwapo kwanza wanajeshi wake wataondoka katika maeneo ya Ukraine inayoidhibiti. 

Vita vya Urusi nchini Ukraine vimeendelea kusambaratisha uhusiano wa taifa hilo na nchi za Magharibi ambapo Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema mataifa hayo yanataka kuifanya Urusi kuyanyenyekea.