Vinu bado vimoto Japan
16 Machi 2011Wataalamu wa kampuni inayokisimamia kinu hicho, Tokyo Electric Power, wanasema vyuma vya mafuta katika eneo la kupoesha la kinu nambari 4 cha Fukushima kilichoathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea nchini Japan, huenda vikawa wazi kutokana na moto huo na vikatowa miale zaidi ya nyuklia hewani.
Hapo jana maafisa wa serikali nchini humo waliwaomba wakaazi waliopo umbali wa kilomita 30 kutoka kwenye kinu hicho, wahame au wajifungie ndani baada ya viwango vyenye athari vya miale hiyo ya nyuklia, kugunduliwa, kufuatia miripuko katika vinu nambari 1 na 4.
Janga lililopo Japan limesababisha kushuka kwa masoko ya hisa kote ulimwenguni, huku faharasha ya Nikkei ya Japan ikishuka kwa kiwango kikubwa tangu mwaka 2008 na DAX ya Frankfurt ikishuka kwa asilimia 3. Wakati huohuo hapo jana matetemeko mengine madogo ya ardhi yalidhihirika mashariki mwa nchi hiyo, siku nne baada ya eneo hilo kuathirika na tetemeko kubwa la ardhi lenye viwango vya magnitudi 9.0, na kusababisha kutokea tsunami.
Idadi ya watu waliofariki inatarajiwa kuzidi watu 10,000, huku maafisa wa uokowaji wakiendelea kutafuta maiti.
Mwandishi:Maryam Abdalla/Afpe,Ap,Dpa,Rtre