1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wa nyuklia Japan wazitikisa siasa za Ujerumani

15 Machi 2011

Kuripuka kwa vinu vya nyuklia nchini Japan, kulikotokana na janga la tetemeko la ardhi na tsunami, kumezua mjadala mkali hapa Ujerumani, juu ya hatima ya vinu vya nyuklia vya taifa hili, huku wanasiasa wakitafautiana.

https://p.dw.com/p/10ZI4
Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: dapd

Imesadifu kwamba janga la kuripuka kwa vinu vya nyuklia vya Japan, linatokea wakati majimbo sita ya Ujerumani yakielekea kwenye chaguzi katika miezi michache ijayo.

Hili limezifanya siasa za atomiki ziingie kwenye siasa za chaguzi, hata ndani ya serikali ya mseto wa "Weusi na Manjano", kama inavyojuilikana serikali ya mseto ya vyama vya CSU/CDU na FDP inayoongoza Shirikisho la Ujerumani.

Ni serikali hii hii ambayo, katika majira ya mapukutiko ya mwaka jana, ilipitisha uamuzi wa kuongeza muda wa kutumika kwa vinu vikongwe vya nyuklia kwa miaka mingine 12. Lakini sasa, Kansela Angela Merkel, anasema uamuzi ule unadurusiwa upya, angalau kwa kipindi hiki.

"Jumamosi hii tumeamua kuwa, vinu vyote vya nyuklia vitafanyiwa uchunguzi kwa kuzingatia janga lililowapata wenzetu wa Japan. Katika uchunguzi huu hakuna jambo la kufichwa. Na kwa sababu hii, tunasitisha kidogo ule uamuzi wa kurefusha matumizi ya vinu hivi, angalau kwa miezi mitatu." Amesema Kansela Merkel.

Ndani ya kipindi hiki, timu ya wataalamu itapaswa kuthibitisha usalama wa mitambo yote, kama vile mfumo wa upozaji mashine, ambao unatajwa kuwa kufeli kwake ni miongoni mwa sababu za miripuko ya siku mbili zilizopita kwenye vinu vya Fukushima Daichi, nchini Japan.

Viongozi wa Die Grüne, Claudia Roth na Cem Oezdemir
Viongozi wa Die Grüne, Claudia Roth na Cem OezdemirPicha: dapd

Lakini kwa chama cha upinzani cha ulinzi wa mazingira, Die Grüne, ambacho tangu mwanzo kimekuwa kikipinga matumizi yoyote ya nishati ya atomiki, bado serikali inaichukulia kadhia ya Japan kijuujuu na kisiasa tu.

"Mtu anaweza kutuona kama vile tunaishi kwenye dhana tu, maana hawa jamaa ndio hawa hawa ambao hadi jana walikuwa wakituambia kuwa nishati ya atomiki ni salama. Lakini kile tulichokuwa tukikihofia sisi, ndicho hicho kinachotokea sasa." Amesema mwenyekiti mwenza wa Die Grüne, Cem Özdemir

Mionzi ya nyuklia si jambo linalopendelewa wala linalohimilika kwa wanaadamu, lakini ni bunge la Ujerumani lililopiga kura katika mwezi Oktoba 2010, kuongeza muda wa vinu 17 vilivyo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, huku vikiwemo vile vilivyofikia umri wa miaka 30.

Kiongozi wa SPD, Sigmar Gabriel
Kiongozi wa SPD, Sigmar GabrielPicha: picture alliance/dpa

Kiongozi wa chama cha upinzani cha SPD, Sigmar Gabriel, anasema kwamba, hata huu muda wa miezi mitatu uliowekwa na serikali kudurusu upya vinu hivi, hauna maana panapohusika hatari ambayo inalikabili taifa.

"Kwa mara nyengine tunajifunza kwamba, hicho kinachoitwa kizibo cha vichwa vya nyuklia, si kitu cha kudhania, bali ni kitu cha uhakika, kwamba kinaweza kuzibuka na kusababisha ajali mbaya sana. Kwa hivyo si jambo ambalo mtu anaweza kulidharau, na ndio sababu tunapaswa kuachana kabisa na masuala ya nishati ya atomiki badala ya kuongeza uwezekano wa kuingia hatarini." Amesema Sigmar.

Kwa vyovyote vile, siasa za atomiki zimesadifu kuchanganyika na siasa za uchaguzi nchini Ujerumani. Na kipimo cha kwanza kitakuwa uchaguzi wa wiki mbili zijazo katika jimbo la Baden-Württemberg, ambapo waziri mkuu wa jimbo hilo, Stefan Mappus, kutoka chama cha kihafidhina cha Kansela Merkel, CDU, anapigania tena nafasi hiyo.

Ikiwa Mappus, ambaye amenukuliwa akipuuzia kitisho chochote cha hatari za vinu vya nyuklia, atashindwa, basi utakuwa ujumbe mwengine wa Kansela Merkel, kuwa nyukulia itakuwa silaha nyengine ya kummaliza yeye mwenyewe kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mwandishi: Richard Fuchs/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman