1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwanja wa ndege wa Timbuktu wakombolewa

MjahidA28 Januari 2013

Vikosi vya Ufaransa vikishirikiana na vile vya serikali ya Mali vimefanikiwa kuukomboa uwanja wa ndege wa Timbuktu uliokuwa unashikiliwa na waasi Kaskazini mwa Mali.

https://p.dw.com/p/17SgN
Wanajeshi wa Mali
Wanajeshi wa MaliPicha: Reuters

Kulingana na msemaji wa jeshi la Ufaransa Kanali Thierry Burkhard, wanajeshi wake walisambazwa katika maeneo tofauti kaskazini mwa Mali, ili kutoa nafasi kwa vikosi vya serikali ya nchi hiyo kukomboa miji ya kaskazini kutoka kwa waasi.

Kwa sasa vikosi hivyo vimejikusanya katika jangwa la mji wa Timbuktu baada ya kukomboa uwanja wa ndege wa mji huo kutoka kwa waasi wanaoondoka kwa kushindwa nguvu, katika ngome zao maeneo ya kaskazini waliokuwa wanashikilia kwa takriban miezi 10.

Vikosi vya Ufaransa
Vikosi vya UfaransaPicha: Reuters

Akizungumza na chombo cha habari cha AFP afisa mmoja katika serikali ya Mali amethibitisha kuudhibiti uwanja wa ndege wa Timbuktu huku akisema kuwa hawakupata ugumu wowote katika kufanya hivyo. Waasi mjini Timbuktu wamekuwa wakiwalazimisha wanawake kuvaa hijabu na pia kuwaadhibu kwa kuwapiga mijeledi na mawe wale ambao watapatikana wakienda kinyume na sheria ya Kiislamu iliyowekwa katika eneo hilo.

Waasi hao pia waliharibu nyumba za kale za ibada wakisema haziendani na sheria na matakwa ya Kiislamu. Amadou Alassane Mega ambaye ni mkaazi wa eneo hilo la kaskazini amesema kila wakati wakipatikana wanavuta sigara au kusikiliza muziki walikuwa wakiadhibiwa na waasi. Amadou Alassane anasema kwa sasa ana furaha kwa kuwa waasi wanalipa kwa kile walichokuwa wakiwafanyia.

Waasi wa Mali
Waasi wa MaliPicha: Reuters

Mji wa Gao ni mkubwa kati ya miji sita iliyokombolewa na vikosi vya Ufaransa na Mali tangu Wafaransa walipoanza oparesheni hiyo dhidi ya waasi Januari 11. Waasi walichukua udhibiti wa kaskazini mwa Mali baada ya wanajeshi walioasi kupindua serikali na kusababisha ghasia na msukosuko katika taifa hilo.

Umoja wa Afrika wakutana kwa ajili ya Mali

Huku hayo yakiarifiwa viongozi wa Umoja wa Afrika pamoja na wale wa Magharibi wanakutana hapo kesho kujadili uungwaji mkono kwa wanajeshi wanaotumwa Mali kupambana na waasi. Hii ni baada ya Umoja huo kuomba msaada wa haraka ili kuwapa nguvu wanajeshi wanaokweda huko.

Mwenyekiti wa AU na rais wa Benin Thomas Boni Yayi
Mwenyekiti wa AU na rais wa Benin Thomas Boni YayiPicha: K.Sia/AFP/Getty Images

Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Ramtane Lamamra, amesema ana matumaini matokeo ya mkutano wa kesho yatakuwa ya kuridhisha na kwamba Umoja wa Afrika utatafuta fedha za kufadhili vikosi vya wanajeshi na pia vifaa vya kijeshi.

Wajumbe kutoka Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Uingereza na Marekani wanatarajiwa kushiriki katika kikao cha kesho. Hapo jana Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema wanatarajia kufanya kila wawezalo kuwasaidia raia wa Mali.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika anayeondoka Thomas Boni Yayi ameishukuru Ufaransa kwa kuingilia kati mzozo wa Mali na wakati huo huo akayalaumu mataifa ya Afrika kwa kuchukua muda mrefu kuingilia kati.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/ AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef