1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yawashambulia waasi wa Mali

25 Januari 2013

Ndege za kivita za Ufaransa zimeshambulia ngome mbili za waasi wenye itikadi kali za Kiislamu kaskazini mwa Mali.

https://p.dw.com/p/17RD3
Wanajeshi wa Ufaransa walioko Mali
Wanajeshi wa Ufaransa walioko MaliPicha: Reuters

Shambulio hilo limefanyika wakati ambapo kundi la waasi lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda la Ansar Dine, likiwa limegawanyika katika makundi mawili. Mbali na mashambulizi hayo ya anga, taarifa zinaeleza kuwa vikosi vya Mali vimekuwa vikifanya mauaji, huku moja kati ya makundi ya haki likisema kuwa kiasi watu 31 wameuawa katikati mwa mji wa Sevare na miili yao imetupwa kwenye visima. Duru za jeshi la Mali zimeeleza kuwa mashambulizi hayo ya anga ya usiku kucha yalikuwa yakililenga eneo la Ansongo lililopo umbali wa kilometa 80 kutoka kwenye mji wa Gao pamoja na ngome mbili za waasi karibu na kijiji cha Seyna Sonrai. Kwa mujibu wa duru hizo, ndege za kijeshi za Ufaransa zimefanikiwa kushambulia maeneo hayo ya waasi na kufanya uharibifu mkubwa.

Wanajeshi wa ECOWAS wapelekwa mpakani mwa Niger

Duru za kiusalama za Niger zimethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo. Zaidi ya wanajeshi 2,000 wa Chad na 500 wa Niger wamepelekwa katika eneo la mpakani la Quallam nchini Niger kwa ajili ya kuanzisha operesheni dhidi ya waasi hao. Wanajeshi hao ni sehemu ya kikosi cha Afrika kilichoidhinishwa na Umoja wa Mataifa waliopelekwa Mali kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi cha Ufaransa na kuchukua nafasi ya wanajeshi wa Ufaransa wanaoongoza operesheni za kijeshi nchini humo. Kampuni ya nyuklia ya Ufaransa ya Areva imesema imeimarisha ulinzi katika mgodi wake wa madini ya nyuklia huko Niger. Uamuzi wa Ufaransa kuiingilia Mali kijeshi umeungwa mkono kimataifa. Gunter Nooke, mshauri wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kuhusu masuala ya Afrika, amesema ni sahihi kuwaunga mkono Ufaransa na haiwezekani kuwaacha wanajeshi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS peke yake, bali inahitajika kuwaunga mkono kwa kuwapatia vifaa au mafunzo kwa wanajeshi wa ECOWAS.

Wanajeshi wa ECOWAS wakiwa Mali
Wanajeshi wa ECOWAS wakiwa MaliPicha: Reuters

Ansar Dine wagawanyika

Nchini Mali kwenyewe, kikosi cha kwanza cha wanajeshi 600 kilichoahidiwa na mataifa ya Afrika kukisaidia kile cha Ufaransa, kimewasili eneo la kaskazini ambako makundi yenye mafungamano na Al-Qaeda yanalidhibiti. Wakati hayo yakijiri, kundi la waasi la Ansar Dine limegawanyika, huku tawi la kundi hilo likielezea utayari wake wa kufanya mazungumzo na serikali ya Mali ya kumaliza operesheni zinazofanywa dhidi ya waasi. Katika taarifa yake, tawi lililojitenga la vuguvugu la Kiislamu kwa ajili ya Azawad limeelezea kupinga siasa kali na aina zote za ugaidi na kwamba linataka kupambana na Ansar Dine. Kundi hilo limetoa wito kwa Mali na Ufaransa kuachana na operesheni zake katika maeneo inayoyadhibiti ya Kidal na Menaka. Maafisa wamesema kuwa waasi wameukimbia mji wa Timbuktu kutokana na mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Ufaransa mwishoni mwa wiki iliyopita na kuharibu makao makuu ya waasi hao.

Waasi wa Ansar Dine
Waasi wa Ansar DinePicha: dapd

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Josephat Charo