Ansar Dine wa Mali wagawika
24 Januari 2013Kundi jipya linalojiita Vuguvugu la Waislamu kwa ajili ya Azzawad limetangaza kujitenga na lile la Ansar Dine, ambalo lilikuwa likilitawala eneo la kaskazini mwa Mali tangu Aprili mwaka jana, kabla ya wanajeshi wa Ufaransa kuingia huko tarehe 12 Januari mwaka huu.
Kundi hilo linaongozwa na Alghabasse Ag Intalla, mkuu wa familia kubwa ya Kituareg kutokea mji wa Kidal, na aliyekuwa mpatanishi wa tawi lenye mrengo wa wastani la Ansar Dinne.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo, kundi hilo limesema kwamba linapingana na aina zote za siasa kali na ugaidi na kwamba liko tayari kupambana nazo, likiongeza kwamba linataka kuutatua mzozo wa Mali kwa njia za amani.
Shirika la habari la AFP, linasema kwa kundi hilo la waasi kutumia jina la Azzawad, inaonesha kwa kiasi gani linataka kujitenga na siasa za Tawi la al-Qaida la Kaskazini mwa Afrika, AQIM, linaloshukiwa kuendeshwa zaidi na wageni, na badala yake kujinasibisha na harakati za watu wa kaskazini mwa Mali, jamii ya Tuareg, ambao kwa miongo kadhaa wamepigania uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe.
Taarifa iliyotolewa na kundi hilo lililojitenga imesisitiza kwamba kundi hilo limeundwa na raia wa Mali peke yake na limezitolea wito serikali za Mali na Ufaransa kuacha uadui kwenye maeneo linaloyashikilia ya Menaka na Kidal "ili kutengeneza mazingira ya majadiliano ya kisiasa kwa njia za amani."
Wanajeshi wa Mali washukiwa kuuwa
Tangazo hilo la kujitenga kwa Vuguvugu la Waislamu kwa ajili ya Azzawad kutoka Ansar Dine linakuja katika siku ambayo Shirikisho la Haki za Binaadamu Duniani (FIDH) limetoa taarifa ya uvunjwaji mkubwa wa haki za binaadamu unaoshukiwa kufanywa na jeshi la Mali kwenye maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa za kuaminika zinasema kwamba kiasi cha watu 20 wameuawa kwa makusudi kwenye miji ya Sevare, Niono na kijiji cha Serbala. Mashahidi wanasema wanajeshi wa Mali wanawalenga watu wenye asili ya Kiarabu na Kituareg, wanaowatambua kwa sababu ya ngozi zao. Mmoja wa wakaazi wa huko, Oummul Sall Seck, ameiambia DW kwa njia ya simu kwamba anahofia usalama wake si kwa sababu ya wanamgambo wa Kiislamu bali kutoka wanajeshi wa serikali.
"Jeshi la Mali halipaswi kuwahukumu watu wa kaskazini kwa tuhuma za kushirikiana na waasi wa Kiislamu ati tu kwa sababu ngozi zao zina rangi inayong'ara. Kuna mtu hapa amekatwa koo kwa sababu tu ya uvumi kwamba alikuwa anashirikiana na Waislamu wenye siasa kali. Hilo si jambo la kawaida!" Amesema Oummul Sall Seck.
Ufaransa yajitenga na visa hivyo
Shirikisho la FIDH limesema pia kwamba limepokea taarifa za uhakika kwamba wanajeshi wa Mali wamehusika kwenye visa vya ubakaji karibu na kijiji kimoja karibu na mji wa Sevare, ambao kwa sasa unashikiliwa na wanajeshi hao baada ya wanajeshi wa Ufaransa kuondoka.
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, amesema kwamba heshima ya jeshi la Mali iko hatarini, huku Waziri wake wa Mambo ya Nje, Laurent Fabius, akisema kwamba Ufaransa haiwezi kukubali aina yoyote ya uvunjwaji wa haki za binaadamu. "Jumuiya ya kimataifa itakabiliwa na hali mbaya sana kama ikinasibishwa ni visa hivyo vya uvunjaji haki za binaadamu," amesema Fabius.
Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binaadamu limezitaka serikali za Mali na Ufaransa kufanya uchunguzi huru wa visa hivyo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman