1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa usalama wadhibiti hali Iraq

Amina Abubakar Grace Patricia Kabogo
3 Oktoba 2019

Maeneo mengi mjini Baghdad yalikuwa kimya huku serikali ya Iraq ikiweka hali ya kutotoka nje baada ya siku mbili za maandamano ya kuipinga serikali, kusababisha mauaji ya watu 19 na mamia ya wengine wengi kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/3Qh75
Irak Bagdad | Ausschreitungen und Proteste
Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Maafisa wa usalama walisambazwa katika maeneo yote mjini Baghdad huku magari ya kubebea wagonjwa na magari ya serikali tu yakionekana katika barabara za mji huo. Duru za polisi zilikiambia chombo cha habari cha dpa kwamba barabara kuu inayoikutanisha mkoa wa kaskazini wa Salah el-Din na Baghdad imefungwa kuzuwia magari madogo ma malori kufika katika mji huo mkuu wa Iraq:

Kulingana na kamisheni huru ya kushughulikia haki za binaadamu nchini humo, watu 1,041 wamejeruhiwa tangu kuanza maandamano hayo ya kulalamikia ukosefu wa ajira, rushwa, na huduma mbovu za umma siku ya Jumanne. Kundi hilo limesema waandamanaji 216 wamekamatwa tangu siku hiyo huku 154 kati yao wakiachiwa.

Kando na hilo mawasiliano ya mtandao pia yamekatwa ikiwa ni juhudi za kudhibiti maandamano zaidi kupitia mitandao ya kijamii.

Maandamano hayo yaliyotokea mwaka mmoja baada ya Waziri Mkuu Adel Abdel-Mahdi kuingia madarakani, yalifanyika katika mikoa kadhaa huku maelfu wakishinikiza uwepo wa huduma nzuri zaidi za umma na nafasi za ajira.

Wawakilishi wa waandamanaji waalikwa bungeni kujadili matakwa yao

Irak Baghdad gewaltsame Proteste gegen Regierung
Baadhi ya waandamanaji mjini BaghdadPicha: Reuters/K. al-Mousily

"Sisi sio adui ya serikali," alisema Sattar al-Obeidi, kijana wa miaka 27 anayefanya kazi ya ujenzi anakopata mshahara mdogo. Kijana huyo anasema anatafuta kazi itakayoimarisha kipato chake ili aweze kuwahudumia watoto wake wawili.

Sattar al-Obeidi anasema haamini kuwa taifa linalozalisha mafuta kama Iraq linashindwa kutatua matatizo yake.

Aidha muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani umetoa wito wa pande zote mbili kupunguza mivutano na kukataa vurugu.

Kulingana na shirika la habari la Iraq msemaji wa bunge Mohammed al Halbusi amewaalika wawakilishi wa maandamano kwenda bungeni kujadili matakwa yao. Hakuna habari zaidi zilizotolewa juu ya hilo lakini inaonekana kuwa ni juhudi za serikali kuidhibiti hali.

Kwa upande wake serikali ya Iraq imesema vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu vimepunguza kasi ya upatikanaji wa miundo mbinu na ajira katika taifa hilo linalokumbwa na vita. Huku hayo yakiarifiwa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran imewatahadharisha mahujaji wake kutoyatembelea maeneo matakatifu ya waumini wa Kishia kufuatia mgogoro huo uliopo katika nchi jirani ya Iraq.

Taarifa kutoka katika wizara hiyo imewataka mahujaji kusubiri hadi usalama urejee nchini Iraq. Kila mwaka mahujaji milioni 2 kutoka Iran wanaitembelea miji mitakatifu ya Washia nchini Iraq kila Oktoba 19.

Vyanzo: dpa,reuters,afp