Usafirisha haramu wa watu wanawiri kufuatia COVID-19
2 Julai 2021Ikitoa ripoti yake ya mwaka 2021 kuhusu biashara ya magendo ya kusafirisha watu kinyume na sheria, wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema wakati serikali zikielekeza nguvu na rasilmali katika sekta ya afya kudhibiti janga la COVID-19, walanguzi wa biashara hiyo haramu wanatumia fursa hiyo kuwasafirisha watu walio katika mazingira magumu.
Wizara hiyo pia ilishutumu baadhi ya nchi lakini pia ikapongeza baadhi ya mataifa kuhusu juhudi zao kukabili ulanguzi wa wanaadamu.
Idadi ya watu katika hatari ya kusafirishwa kimagendo yaongezeka
Ripoti hiyo ya kila mwaka imeeleza kwamba janga la COVID-19 lilitengeneza mazingira ambapo idadi ya watu walioko katika mazingira magumu na kujikuta katika hatari ya walanguzi wa wanadamu, iliongezeka.
Soma pia: Nguvu zaidi zahitajika kukabiliana na ulanguzi wa binadamu
Aidha janga hilo lilivuruga mifumo ambayo ilishawekwa zamani ya kupambana na biashara hiyo haramu.
"Serikali kote ulimwenguni zilitoa nguvu zao kwingineko na kuzielekeza hasa dhidi ya janga la COVID-19. Mara nyingi hatua hiyo ilífanya juhudi za kupambana na usafirishaji wa wanadamu kuwa dhaifu,” ripoti hiyo imesema.
Imeongeza kuwa, wakati hayo yakifanyika, walanguzi walizidisha juhudi zao kuwalenga watu katika mazingira magumu kutokana na hali mbalimbali ikiwemo janga la virusi vya corona.
Kari Johnstone, ambaye ni mkurugenzi katika ofisi inayofuatilia na kupambana na magendo ya kusafirisha watu, amesema hali hizo kwa pamoja zilisababisha mazingira ya usafirishaji wanaadamu kunawiri.
Wasichana wadogo waacha shule na kuozwa kwa lazima
Ripoti hiyo ilitolea mfano nchi za India na Nepal ambako wasichana kutoka família masikini vijijini mara kwa mara walitarajiwa kuacha shule kusaidia katika juhudi za kutafuta riziki kwa família zao kufuatia hali ngumu za kiuchumi.
Wanawake wa Korea Kaskazini wageuzwa watumwa wa ngono China
Ripoti imeeleza kwamba baadhi yao waliozwa kwa lazima ili familia zao zipate hela, na wengine walilazimishwa kufanya kazi ili kuongeza mapato nyumbani baada ya wazazi wao kupoteza ajira kutokana na janga la COVID-19.
Katika mataifa mengine, wamiliki wa majumba ya kukodisha walifanya mapenzi na wapangaji wao wa kike kwa lazima baada ya wao kushindwa kulipa kodi.
Aidha katika nchi nyingine magenge yaliwavamia wahamiaji katika kambi za wakimbizi.
Nchi sita zashushwa daraja ikiwemo Israel
Ripoti hiyo huorodhesha mataifa kote ulimwenguni kulingana na utekelezaji wao wa sheria ya kimataifa yam waka 2000, dhidi ya usafirishaji haramu wa wanadamu.
Cyprus, Israel, New Zealand, Norway, Ureno na Switzerland zilishushwa ngazi katika mapambano yao dhidi ya kadhia ya ulanguzi wa wanadamu, hivyo yalitolewa katika kundi la kwanza hadi kundi la pili
Kundi la pili hujumuisha nchi ambazo hazijatimiza kikamilifu sheria ya kimataifa ya kupambana na usafirishaji wa wanadamu. Lakini zinapiga hatua kubwa kujaribu kutimiza sheria hiyo.
Mataifa mawili, Guinea Bissau na Malaysia yaliongezwa katika kundi la tatu, ambalo ni la mataifa yenye rekodi mbaya zaidi katika vita dhidi ya ulanguzi wa wanadamu. Mataifa kwenye kundi hilo ni pamoja na Afghanistan, Algeria, Burma, China, Comoros, Cuba, Eritrea, Iran, Nicaragua, Korea Kaskazini, Urusi, Sudan Kusini, Syria, Turkmenistan na Venezuela.
Nchi nne; Belarus, Burundi, Lesotho na Papua New Guinea ziliondolewa katika kundi la tatu na kupandishwa ngazi hadi kundi la pili.
Adhabu ya Marekani kwa nchi zenye sifa mbaya za ulanguzi wa watu
Marekani huweza kuzuia misaada yoyote ya kigeni kwa mataifa yaliyoko kwenye kundi la tatu, ikiwa rais ataridhia.
Uturuki, ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, ilitajwa kuwa na visa vingi vya ukiukwaji wa sheria inayozuia utumikishwaji wa watoto jeshini hasa kufuatia hatua ya Uturuki kuunga mkono makundi ya Syria na Libya yanayowatumia watoto jeshini.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema, wanatumai Uturuki itawahimiza washirika wake wanaohusishwa na machafuko ya Syria na Libya kukoma kuwatumikisha watoto jeshini.
(AFPE)