1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wa Korea Kaskazini wageuzwa watumwa wa ngono China

John Juma Mhariri: Sekione Kitojo
21 Mei 2019

Ukandamizaji wa kingono unaofanywa dhidi ya Wakorea wa Kaskazini huyapa magenge ya China faida ya dola milioni 105 kila mwaka.

https://p.dw.com/p/3IqVE
China Prostitution
Picha: picture alliance/ROPI

Wataalamu wamesema kuwa maelfu ya wanawake na wasichana kutoka Korea Kaskazini, wanapojaribu kukimbia umaskini na ukandamizaji nchini mwao, wanasafirishwa kimagendo kuelekea China ambapo wanageuzwa kuwa watumwa wa kingono.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali kwa jina Korea Future Initiative lenye makao yake mjini London, ukandamizaji wa kingono unaofanywa dhidi ya Wakorea wa Kaskazini huyapa magenge ya China faida ya dola milioni 105 kila mwaka. Hiyo ikiwa ni kando na mateso wanayoyapitia wanawake wanaosafirishwa kimagendo.

Waathirika ambao ni wanawake na wasichana, wengine wakiwa na umri mdogo wa miaka 9, hushirikishwa kwenye ukahaba na kulipwa pesa kidogo dola 4.30.  Wengine huuzwa kuolewa kwa yuan 1000. Wanatumikishwa kingono na video zao za ngono husambazwa kwenye mitandao. Amesema Yoon Hee-soon aliyeiandika ripoti hiyo.

Ameongeza kuwa wengine huuzwa zaidi ya mara moja na hulazimishwa katika utumwa wa kingono angalau kwa mwaka mmoja wakiwa nje ya nchi yao.

Wengi wa waathiriwa husafirishwa China Kimagendo

Ripoti yasema baadhi ya wanawake wamekufa kutokana na magonjwa ya zinaa au mateso.
Ripoti yasema baadhi ya wanawake wamekufa kutokana na magonjwa ya zinaa au mateso.Picha: STR/AFP/Getty Images

Kulingana na ripoti ambayo inapaswa kuzinduliwa Jumatatu katika bunge la Uingereza, inakadiriwa kuwa asilimia 60 ya wasichana na wanawake wa Korea Kaskazini walioko China husafirishwa kimagendo kutumikishwa kwenye biashara ya ngono.

Watafiti wameeleza kuwa nusu ya wanawake na wasichana hao hulazimishwa kwenye ukahaba. Theluthi moja huuzwa ili kuolewa na wengne wengi hushirikishwa kwenye ngono kupitia intaneti.

Shirika la habari la Reuters limesema hakukuwa na afisa yeyote wa China katika ubalozi wao mjini London kuzungumzia suala hilo.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Wakorea wengi wa Kaskazini ni watumwa katika madanguro katika wilaya za kaskazini mashariki mwa China iliyo na wahamiaji wengi.

Waathiriwa wafariki kutokana na magonjwa ya zinaa

Waathiriwa wa biashara hiyo haramu wanasema makahaba mjini Shangai waliwekewa tattoos za michoro kama ya simba na vipepeo kuonyesha nani anawamiliki na pia kuwaepusha dhidi ya kutekwa na magenge pinzani.

Waliohojiwa walieleza visa vya baadhi ya wanawake kufariki kutokana na magonjwa ya zinaa na mateso.

Wasichana wanaoshirikishwa kwenye ngono mitandaoni aghalabu huwa na umri wa kati ya miaka 12 na 29, lakini wakati mwingine hata walio na umri wa miaka ya chini zaidi. Ripoti hiyo imeeleza.

Wanalazimishwa kufanya vitendo vya ngono au wanadhulumiwa kingono huku video zao zikichukuliwa. Wakati mwingine visa hivyo hupeperushwa moja kwa moja katika tovuti za ngono.

Vyanzo: Reuters