1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yataka Ukraine ichunguzwe kuhusu silaha za kibayolojia

2 Novemba 2022

Baraza la Usalama la UN kupiga kura kuhusu azimio la kuunda tume ya kuchunguza madai ya Urusi kwamba Ukraine na Marekani zinatengeneza silaha za kibaolojia zinakiuka mkataba unaozuia matumizi ya silaha za kibaolojia.

https://p.dw.com/p/4Ix8A
UN - Mehrheit verurteilt Annexionen Moskaus
Picha: David Delgado/REUTERS

Wiki iliyopita, Urusi ilisambaza kwa wanachama wa Baraza La usalama la Umoja wa Mataifa, taarifa yenye kurasa 310 iliyodai kwamba Ukraine inatengeneza silaha za kibaolojia kwa usaidizi wa jeshi la Marekani.

Taarifa hiyo ilijumuisha malalamishi kwa baraza hilo chini ya kipengee cha VI cha mkataba wa 1972 kuhusu matumizi ya sihala za kibaolojia. Aidha ilijumuisha muswada ambao unawezesha baraza hilo kuunda tume ya wanachama 15 kuchunguza madai hayo.

Soma pia taarifa isemayo 'Zelensky ataka ulinzi katika usafirishaji nafaka za Ukraine'

Urusi ilidai kuwa kuna maabara ya silaha za kibaolojia za Marekani nchini Ukraine kisiri. Ilitoa madai hayo siku chache tu baada ya kuivamia Ukraine Februari 24.

Hata hivyo madai hayo yamekanushwa na wanasayansi, maafisa wa Ukraine, ikulu ya Marekani na vilevile makao makuu ya jeshi la Marekani Pentagon.

Wanadiplomasia wamesema kuna uwezekano mkubwa kwamba azimio hilo la Urusi halitapitishwa kwenye kura mchana wa leo. Ili liidhinishwe, sharti liungwe mkono na angalau wanachama tisa na kusiwe na hata kura moja ya turufu dhidi yake kutoka kwa wanachama wa kudumu ambao ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield asema madai ya Urusi kuhusu uwepo wa maabara za silaha za kibaolojia nchini Ukraine ni sehemu ya kampeni yake ya upotoshaji na kuwafumba watu macho dhidi ya maovu ya jeshi la Urusi nchini Ukraine.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield asema madai ya Urusi kuhusu uwepo wa maabara za silaha za kibaolojia nchini Ukraine ni sehemu ya kampeni yake ya upotoshaji na kuwafumba watu macho dhidi ya maovu ya jeshi la Urusi nchini Ukraine.Picha: David Delgado/REUTERS

IAEA yaanza ukaguzi juu ya "mabomu machafu" Ukraine

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alitaja kura hiyo iliyoitishwa na Urusi kama kupoteza muda. Aliyapinga madai ya Urusi kwa kusema ni uwongo mtupu ambayo ni sehemu ya kampeni ya Urusi ya kueneza taarifa za kupotosha, na kuwafanya watu wasiangazie dhuluma ambazo wanajeshi wake wanafanya nchini Ukraine. Ameongeza kuwa madai ya Urusi ni mbinu ya kuthibitisha vita vyake nchini Ukraine.

"Ukraine haina mpango wa silaha za kibaolojia. Marekani vilevile haina mpango wa silaha za kibaolojia. Hakuna maabara ya silaha za kibaolojia za Ukraine zinazosaidiwa na Marekani,” amesema Thomas-Greenfield.

Usafirishaji nafaka kutoka Ukraine waendelea licha ya kujitoa kwa Urusi

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia aliishutumu Marekani kwa kufanya kazi nchini Ukraine ya kutengeneza vimelea hatari vinavyoua, ikiwemo virusi vinavyosababisha kipindupindu, tauni, kimeta na homa nyinginezo. Aliongeza kuwa nyaraka na ushahidi ambao maafisa wa Urusi walipata ulidokeza jeshi linahusika katika shughuli hizo.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia amedai jeshi la Urusi nchini Ukraine limepata nyaraka za utafiti kuhusu uwezekano wa kutumia popo na ndege wa kuhamahama kusambaza virusi hatari alivyodai vinatengenezwa kwenye maabara Ukraine.
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia amedai jeshi la Urusi nchini Ukraine limepata nyaraka za utafiti kuhusu uwezekano wa kutumia popo na ndege wa kuhamahama kusambaza virusi hatari alivyodai vinatengenezwa kwenye maabara Ukraine.Picha: Yuki Iwamura/AP/picture alliance

Nebenzia aliliambia Baraza la Usalama kwamba katika kipindi ambacho jeshi la Urusi limekuwa Ukraine, limekamata ndege zisizohitaji rubani yaani droni zenye uwezo wa kufanya mashambulizi ya virusi hivyo. Na pia wamepata nyaraka zinazohusishwa na utafiti wa uwezekano wa kusambaza virusi hivyo kutumia popo na ndege wengine wa kuhama hama.

Urusi yaendeleza mashambulizi miji ya Ukraine

Thomas-Greenfield alipinga madai hayo ya Urusi na kusema yanasikitisha kwa sababu nyingi ikiwemo, ikiwa wanyama na ndege wangetumiwa kusambaza virusi hivyo, basi hiyo itakuwa hatari kwa bara zima la Ulaya, dhidi ya Ukraine yenyewe na kwa nchi yoyote ile.

Mnamo Septemba mwaka huu, nchi 197 wanachama wa mkataba kuhusu silaha za kibaolojia walikutana kufuatia ombi la Urusi, kujadili shughuli katika maabara ya kibaolojia nchini Ukraine. Hata hivyo ripoti ya mkutano huo ilisema haikuwezekana kupata maafikiano ya pamoja.

Ukraine ina mtandao wa maabara ya kibaolojia ya utafiti na hufadhiliwa na Marekani. Husimamiwa na Ukraine kama sehemu ya mkakati wa kupunguza kitisho cha kibaolojia unaolenga kupunguza hatari endapo kuna miripuko ya maradhi iwe ya kawaida au iliyochochewa na wanadamu.

(APE)