1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA yaanza ukaguzi juu ya "mabomu machafu" Ukraine

1 Novemba 2022

Shirika la kimataifa la kudhibiti nguvu za Atomiki, IAEA limesema limeanzisha ukaguzi nchini Ukraine kama sehemu ya uthibitisho huru wa madai ya Urusi kwamba ukraine inataka kutumia kile ilichokitaja mabomu machafu.

https://p.dw.com/p/4IuQ9
Rafael Grossi | IAEO Direktor | Pressekonferenz UNO in New York
Picha: Luiz Rampelotto/ZUMA Wire/IMAGO

Kulingana na shirika hilo la IAEA wataalamu wake wameanzisha ukaguzi ambao utamalizika hivi karibuni, ili kujithibitishia madai hayo kwenye maeneo mawili nchini Ukraine. Taarifa imesema, mkurugenzi wa shirika hilo Rafael Grossi baadaye wiki hii atatoa hitimisho lake la awali kuhusiana na kile kilichoonekana.

Ukaguzi huo unafuatia ombi la maandishi kutoka kwa serikali ya Ukraine la kupeleka timu ya ukaguzi kwenye maeneo hayo. Urusi imeishutumu Ukraine kwa kujiandaa kutumia mabomu hayo dhidi ya wanajeshi wake, huku Kyiv kwa upande wake ikidai kwamba, Urusi ndio inajiandaa kutumia mabomu hayo.

Soma Zaidi: Ukraine yaupoteza mji wa Lysychansk

Shirika hilo lilisema wiki iliyopita kwamba limekagua moja ya maeneo hayo mawili mwezi mmoja uliopita, lakini hakukuonekana shughuli yoyote ya nyuklia ama vifaa vinavyohusiana na shughuli hizo na Alhamisi wiki iliyopita, rais Vladimir Putin wa Urusi alitoa mwito kwa shirika hilo kufanya ukaguzi haraka nchini Ukraine.

Griechenland | PK Olaf Scholz und Kyriakos Mitsotakis in Athen
kansela wa ujerumani Olaf Scholz ayapuuza madai ya Urusi kuhusiana na mabomu machafuPicha: Michael Varaklas/AP Photo/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Sholz ameyaelezea madai hayo ya Urusi dhidi ya Ukraine kuwa yasiyo ya msingi, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa serikali Steffen Hebestreit, jana usiku baada ya Scholz kuzungumza kwa simu na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky. Amesema, kansela anaunga mkono hatua hiyo ya IAEA na ana matumaini kwamba itaondoa shakashaka juu ya madai hayo ya Urusi.

Aidha wakuu hao wawili walitoa mwito wa utekelezaji pamoja na kuongeza muda wa makubaliano ya nafaka chini ya Umoja wa Mataifa ili kupunguza wasiwasi ulioanza kujitokeza. Hata hivyo, taarifa zimesema meli za nafaka kupitia Bahari Nyeusi zimeendelea kusambaza chakula licha ya hatua ya Urusi kusitisha makubaliano ya usambazaji, hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo rais Putin amesisitiza kwamba hawajajitoa kwenye makubaliano hayo, bali wamesitisha tu.

Russland I Vladimir  Putin
Rais Vladimir Putin amesisitiza kwamba hawajajitoa kwenye makubaliano ya kusafirisha nafaka. Picha: Sergei Karpukhin/AP/picture alliance

"Kwa hivyo hatusemi kwamba tunajiondoa katika mpango huu. Hapana..., tunasema kwamba tunasimamisha. Mmoja wa waandaaji wa mpango huu alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wanashiriki kikamilifu katika mchakato huu, na tunawashukuru, bila shaka. Sasa waendelee kuwasiliana na Ukraine, ili Ukraine ihakikishe kwamba hakutakuwa na hatari yoyote." Alisema Putin.

Soma Zaidi: Usafirishaji nafaka kutoka Ukraine waendelea licha ya kujitoa kwa Urusi

Meli 12 ziliondoka kwenye bandari za Ukraine jana Jumatatu na mbili zilielekea Ukraine kujaza chakula kingine.

Katika hatua nyingine, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema mashambulizi kwenye miundombinu ya Ukraine kwa sehemu ni ulipizaji kisasi dhidi ya hatua ya Ukraine ya kuzishambulia meli zake kwenye Bahari Nyeusi mwishoni mwa wiki iliyopita. Amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari uliorushwa kwenye televisheni kwamba pengine wasingeishia hapo, hali inayoashiria mashambulizi zaidi yanaweza kufuata.

Urusi iliishambulia kwa makombora mitambo ya kusambaza nishati katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na kusababisha karibu maghorofa 250,000 kukosa umeme usiku wa jana. Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko alisema mji huo kwa kiasi bado hauna huduma za maji, ingawa ameahidi kurejesha taratibu huduma hizo hii leo pamoja na kutangaza hatua kadhaa zitakazosaidia kupunguza matumizi ya nishati ya umeme.

Mashirika