1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaupoteza mji wa Lysychansk

4 Julai 2022

Ukraine yaupoteza mji wa Lysychansk kwa wanajeshi wa Urusi wakati viongozi mbali mbali duniani wakijiandaa huko Uswisi kutangaza mpango wa kuisaidia nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita.

https://p.dw.com/p/4DcG6
Ukraine | Krieg | Soldaten in Lyssytschansk
Picha: Rick Mave/ZUMAPRESS/picture alliance

Vikosi vya Urusi vimejaribu leo kuongeza mashambulizi yao katika eneo la Mashariki mwa Ukraine baada ya kulidhibiti eneo la nchi hiyo. Kwa upande mwingine Jeshi la Ukraine limedhibitisha kwamba vikosi vyake vimeondoka kwenye mji wa Lysychansk katika mkoa wa Luhansk. Wakati huohuo nchi za Magharibi zinaendelea kulaani mashambulizi ya Urusi ndani ya Ukraine.

Mji wa Lysychansk ndio eneo la mwisho ambako wanajeshi wa Ukraine bado walikuwa wakilipigania katika mkoa wa Luhansk, moja ya mikoa miwili ambayo ndiyo inayounda eneo zima la mashariki la Donbass linalofahamika kwa shughuli za kiviwanda nchini Ukraine.

Russia Ukraine War
Picha: Luhansk region military administration/AP/picture alliance

Wanajeshi wa Urusi sasa wanadhibiti pia kiasi nusu ya mkoa wa Donetsk ambao ndio mkoa wa pili kwenye eneo hilo la Donbas.Jeshi la Ukraine limeripoti kwamba hivi sasa wanajeshi wa Urusi wanazilenga harakati zao kuelekea upande wa miji ya Siversk,Fedorivka na Bakhmut iliyoko katika mkoa wa Donesk. Kadhalika wanajeshi hao wa Urusi wameongeza mashambulizi dhidi ya miji muhimu ambayo bado iko mikononi mwa wanajeshi wa Ukraine ya Sloviansk na Kramatorsk katika mkoa wa Donetsk.

Jana Jumapili watu sita akiwemo mtoto wa kike wa miaka 9 waliuliwa katika mashambulizi ya mabomu ya wanajeshi wa Urusi  na watu wengine 19 walijeruhiwa kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo. Rais Vladmir Putin alishaweka wazi kwamba kulitwaa eneo zima la Donbass ndio lengo muhimu katika vita vyake nchini Ukraine ambavyo sasa viko katika mwezi wake wa tano.

Paris Viva Technology Konferenz Selenzky Hologram
Picha: Benoit Tessier/REUTERS

Waasi wanaoungwa mkono na Urusi katika eneo hilo la Donbass wamekuwa wakipambana na wanajeshi wa Ukraine tangu mwaka 2014 baada ya kujitangazia uhuru wao wa kujitenga na Ukraine baada ya Urusi kulinyakua kwa mabavu jimbo la Crimea. Na ikumbukwe kwamba Urusi ilitangaza kutambua uhuru wa majimbo yote ya Donbass yaani Luhansk na Donetsk siku chache kabla haijaivamia Ukraine Februari 24.

Jana waziri wa ulinzi wa Urusi aliripoti kwa rais Putin kwamba jeshi la Urusi na washirika wao yaani waasi wa mashariki sasa wanakamata udhibiti wa jimbo la Luhansk baada ya kutwaa udhibiti kamili wa mji wa Lysychansk.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekiri kuondoka kwa wanajeshi wake ingawa ameapa kwamba vikosi vya nchi yake vitaendelea kupambana.Hii leo rais Zelensky anatarajiwa kuwatuhubia viongozi  kutoka nchi mbali mbali na mashrika ya ulimwengu huko Uswizi ambako utatangazwa mpango maalum wa kusaidia kuijenga upya nchi yake.Lakini tayari ameshatowa tahadhari kwa viongozi hao kwamba kuna kazi kubwa ya kufanyika.

Na wajumbe wa nchi za Magharibi nchini China wameikosoa sana Urusi leo Jumatatu kwa uvamizi wake Ukraine ambapo balozi wa Marekani Beijing, Nicholas Burns amesema China haipaswi kuendeleza Propaganda za Urusi katika kongamano la hadhara ambalo sio la kawaida na hasa kwakuwa China imekataa kulaani mashambulizi ya Urusi.

USA US-Botschafter in China nominiert Nicholas Burns
Picha: Rod Lamkey/CNP/picture alliance

Balozi Burns ametoa kauli hiyo akizungumza mbele ya kongamano la amani la dunia lililoandaliwa na chuo kikuu cha Tsinghua, na kuongeza kusema kwamba vita vya Urusi dhidi ya Ukraine ni kitisho kikubwa kwa amani ya dunia na China haipaswi kuendeleza Propaganda za Urusi za kuilaumu jumuiya ya kujihami ya Nato kuhusu vita hivi.

Mabalozi wa Uingereza na Ufaransa pia wameikosoa Urusi kwenye kongamano hilo la mabalozi wa kigeni nchini China, wasomi na wanafunzi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW