1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMsumbiji

Msumbiji: Upinzani watoa wito kuomboleza vifo vya watu 50

20 Novemba 2024

Kiongozi wa upinzani nchini Msumbiji Venancio Mondlane ametoa wito wa kuanzisha siku tatu za maombolezo kuanzia leo Jumatano kutokana na vifo vya watu 50 aliosema waliuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi wa Oktoba 9.

https://p.dw.com/p/4nBP3
Msumbiji: Waandamanaji wakiwa na picha ya Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane
Waandamanaji wakiwa na picha ya Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji Venancio MondlanePicha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Katika chapisho kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mondlane ametaka pia kuhesabiwa upya kwa kura baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Daniel Chapo wa chama cha Frelimo kilichopo madarakani kwa karibu nusu karne kuwa mshindi.

Rais wa Msumbiji  Filipe Nyusi anayetakiwa kuondoka madarakani mwezi Januari amelihutubia taifa siku ya Jumanne na kulaani "jaribio la kuanzisha machafuko katika nchi hiyo" huku akihimiza kufanyike mazungumzo ili kumaliza machafuko yaliyodumu kwa wiki kadhaa.

Viongozi wa SADC kujadili ghasia za Msumbiji

Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)Picha: Tafara Mugwara/Xinhua/IMAGO

Hayo yanajiri wakati viongozi wa nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) watakutana siku ya Jumatano (20.11.2024) mjini Harare kwa mkutano unaotarajiwa kujadili machafuko nchini Msumbiji, miongoni mwa masuala mengine ya kikanda.

Mzozo wa kisiasa na kijamii unaozidi kuongezeka Msumbiji utakuwa ndio ajenda kuu ya mkutano wa kilele wa SADC ulioitishwa baada ya matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 9 kusababisha maandamano ya wiki kadhaa na kumfanya mgombea wa upinzani aliyeshindwa kupinga matokeo.

Soma pia: Mzozo wa kisiasa wa Msumbiji kutawala mkutano wa kilele wa SADC

Watu wasiopungua 30 wanaripotiwa kuuawa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi kufuatia ushindi wa mgombea wa chama tawala cha FRELIMO Daniel Chapo. 

Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane anayapinga matokeo hayo ambayo anadai kuwa yamechakachuliwa na kuitisha maandamano ya nchi nzima. Miito imekuwa ikitolewa ili kurejeshwa hali ya utulivu na utawala wa sheria nchini Msumbiji.