1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMsumbiji

Mkutano wa SADC utamudu kumaliza mzozo wa Msumbiji?

15 Novemba 2024

Zimbabwe, mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ,imesema jumuiya hiyo ya kikanda itakutana mjini Harare kwa mkutano maalumu wa kilele kati ya Novemba 16 na 20.

https://p.dw.com/p/4n3RW
Vurumai ya baada ya uchaguzi mkuu nchini Msumbiji
Vurumai ya baada ya uchaguzi mkuu nchini Msumbiji Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Wakati wa mkutano huo wa mataifa 16 yanayozijumuisha Angola, Botswana, Visiwa vya Comoros, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Ushelisheli, Tanzania, Zambia na  Zimbabwe, suala kuu katika agenda litakuwa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji.

Piers Pigou, mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika Taasisi ya mafunzo ya usalama ISS mjini Pretoria, Afrika Kusini, ameiambia DW kwamba awali mkutano huo wa kilele wa SADC ulikuwa umepangwa kushughulikia masuala yanayohusiana na jinsi hali ilivyo katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Huko jumuiya hiyo imetuma vikosi vyake kuvisaidia vikosi vya nchi hiyo kukabiliana na waasi wa M23 pamoja na makundi mengine yenye silaha mashariki mwa Kongo.  

Lakini kutokana na matukio ya baada ya uchaguzi wa mwezi uliopita nchini Msumbiji,Jumuiya hiyo inatarajiwa kushughulikia hali hiyo ama pia kusikia kutoka kwa rais wa nchi hiyo Filipe Nyusi kuhusu kinachoendelea na hatua wanazochukuwa.

Mashirika yanasema watu 30 wameuawa Msumbiji tangu kuzuka ghasia za baada ya uchaguzi 

Bendera za baadhi ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya SADC
Bendera za baadhi ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya SADC.Picha: Borralho Ndomba/DW

Kulingana na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, takriban watu 30 wameuawa nchini Msumbiji baada ya takriban wiki tatu za maandamano kufuatia uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata wa Oktoba 9.

Wiki hii, kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane alitoa wito wa maandamano mapya kuhusiana na matokeo ya uchaguzi huo licha ya msako mkali wa polisi na kupelekwa kwa maafisa wa jeshi kukabiliana na maandamano hayo.

Mondlane, aliyeibuka wa pili baada ya ushindi wa mgombea wa chama tawala cha Frelimo Daniel Chapo, amepinga vikali matokeo hayo ya uchaguzi aliyoyataja kukumbwa na kasoro kubwa za uchaguzi.

Linda Masarira, kiongozi wa kisiasa wa upinzani nchini Zimbabwe aliyegombea urais wakati wa uchaguzi wa mwaka 2023 nchini humo, ameiambia DW kwamba jumuiya ya SADC haijawajibika ipasavyo na kwamba wakati wote imekuwa kimya linapokuja suala la mizozo ya uchaguzi akiongeza kuwa hali hiyo inaibua maswali kuhusu kujitolea kwake katika kukabiliana na masuala ya uchaguzi.

Upinzani nchini Msumbiji pia umeushtumu ujumbe wa uangalizi wa uchaguzi wa jumuiya hiyo SEOM baada ya kupongeza mchakato huo wa uchaguzi.

Waangalizi wa kimataifa ikiwa ni pamoja na wale wa Umoja wa Ulaya, walihitimisha kuwepo kwa kasoro kubwa za uchaguzi.

Jumuiya hiyo itamudu kumaliza machafuko Msumbiji?

Viongozi wa nchi za SADC
Viongozi wa mataifa wanachama wa SADC kwenye moja ya mikutano ya kilele ya jumuiya hiyo ya kikanda.Picha: Tafara Mugwara/Xinhua/IMAGO

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa atakayeongoza mkutano huo wa SADC alikuwa mmoja kati ya viongozi wa kwanza wa mataifa kumpongeza Chapo kwa ushindi wake wa uchaguzi.

Polisi yatawanya waandamanaji kwa gesi ya machozi Msumbiji

Upinzani ulimshtumu haraka kiongozi huyo wa Zimbabwe kwa hatua hiyo aliyochukuwa hata kabla ya Tume ya uchaguzi (CNE) kutangaza matokeo ya mwisho.

Kufanya hali kuwa ngumu zaidi, Baraza la Katiba la nchi hiyo bado halijaidhinisha matokeo hayo huku wakati ambapo kuna kesi za kisheria zilizowasilishwa na vyama vya upinzani.

Swali ni je? SADC imeungana kwa kiasi gani katika azma yake ya kuufikisha mzozo wa kisiasa nchini Msumbiji?

Pigo anasema huenda kuna dhana kama hiyo wakati ambapo uongozi wa Angola, Tanzania, Afrika Kusini na Zimbabwe tayari umeipongeza Frelimo na mgombea wake wa urais, wakati mataifa mengine yanasubiri kukamilika kwa mchakato huo wa matokeo ya mwisho na kuongeza kuwa pongezi hizo za mapema, haziashirii mgawanyiko wowote mkubwa ndani ya SADC.

Pigo ameongeza kuwa SADC itajikakamua kuwa na msimamo wa pamoja miongoni mwa mataifa wanachama.