UN: Pande zote mzozo wa Ukraine zauwa raia
3 Februari 2015Hayo yamesemwa na mkuu wa shirika la Umoja huo linalohusika na haki za binadamu Zeid Ra'ad al Hussein, ambaye ameongeza kuwa mnamo wiki tatu zilizopita, watu wasiopungua 224 wameuawa mashariki mwa Ukraine.
Zeid Ra'ad al Hussein amesema katika taarifa yake kwamba vituo vya mabasi ya usafiri wa umma, masoko, shule, hospitali na mitaa yenye makaazi ya watu vimegeuzwa uwanja wa mapigano mashariki mwa Ukraine, na kwamba idadi ya watu waliopoteza maisha katika vita hivyo vya miezi takribani kumi imepindukia 5,350. Pamoja na watu 224 waliouawa mnamo wiki tatu zaidi zilizopita, wengine 545 wamejeruhiwa katika mapigano, amesema mkuu huyo wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na haki za binadamu.
Ujerumani yasisitiza haitaipa silaha Ukraine
Huku hayo yakiarifiwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amerudia kauli yake kwamba Ujerumani haina mpango wa kuipa Ukraine msaada wa silaha za kivita, akisisitiza kuwa diplomasia na vikwazo ndio njia muafaka ya kuusuluhisha mgogoro wa nchi hiyo.
''Ujerumani haitaipa Ukraine silaha ya kivita, hayo niliyasema jana. Tunaweka juhudi katika kutafuta suluhisho la kidiplomasia, na waziri wa mambo ya nchi za nje ameeleza bayana kwamba ikiwa hali itadhihirika kuendelea kuwa mbaya, tutalazimika kuweka vikwazo vipya kwa Urusi''. Amesema Bi Merkel.
Lakini tofauti na Ujerumani, Marekani imesema inatafakari uwezekano wa kuipa Ukraine zana za kivita. Hata hivyo kulingana na afisa ya ngazi ya juu wa utawala wa rais Barack Obama, hakuna uhakika juu ya iwapo uamuzi wa kutoa silaha kwa nchi hiyo utafikiwa. Waziri wa Mambo ya Nchi za nje wa Marekani John Kerry anatarajiwa kufanya ziara mjini Kiev siku ya Alhamis, ambapo mawaziri wa wa ulinzi wa nchi wanachama wa umoja wa kujihami-NATO watakuwa wakikutana mjini Brussels.
Hakuna atakaye vita vya mawakala
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Jen Psaki, amesisitiza hata hivyo kuwa hakuna aliye na hamu ya kuanzisha vita vya kutumia mawakala kati ya Marekani na Urusi. ''Madhumuni yetu ni kuilazimisha Urusi kubadilisha mwenendo wake, na hiyo ndio sababu tumeiwekea nchi hiyo vikwazo'', amesema Psaki.
Uhasama uliibuka upya mwezi Januari baina ya wanajeshi wa Ukraine na waasi wa mashariki wanaotaka kujitenga, baada ya hali ya utulivu iliyoshuhudiwa mwezi Desemba. Duru nyingine ya mazungumzo ilivunjia Jumamosi iliyopita, huku kila upande ukiutuhumu mwingine kutaka kurefusha mzozo ulioanza mwezi Aprili mwaka jana.
Mashambulizi mapya ya waasi kwa sasa yanaelekezwa katika mji wa Debaltseve kwenye njia panda ya reli iliyo kati ya miji ya Donetsk na Luhansk ambayo inadhibitiwa na waasi mashariki mwa Ukraine. Wakazi 2000 wameuhama mji huo mnamo siku chache zilizopita.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre/afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman