1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo mapya ya amani ya Ukraine

30 Januari 2015

Wapatanishi kutoka Ukraine, Urusi na Ulaya wanajiandaa kwa mazungumzo mapya ya amani katika juhudi za kukomesha mapambano kati ya serikali ya Ukraine na waasi wanaoungwa mkono na Urusi.

https://p.dw.com/p/1ETL5
Wanajeshi wa Ukraine katika mji wa Luhansk mashariki mwa Ukraine.
Wanajeshi wa Ukraine katika mji wa Luhansk mashariki mwa Ukraine.Picha: Reuters/M. Levin

Mazungumzo hayo yaliopangwa kufanyika katika mji mkuu wa Belarus Minsk Ijumaa (30.01.2015) yatazikutanisha pamoja kundi la mawasiliano la wawakilishi wa Ukraine,Urusi na Shirika la Usalama na Ushirikiano la Umoja wa Ulaya (OSCE).

Lakini mkutano huo unatarajiwa kutiwa kiwingu na makubaliano yaliofikiwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya hapo jana kuimarisha vikwazo dhidi ya Urusi kutokana na mzozo huo ambapo Umoja wa Mataifa unasema umeuwa zaidi ya watu 5,100.

Kiongozi wa zamani wa Urusi Mikhail Gorbachov ameonya hapo jana kwamba vikwazo hivyo vinahatarisha kuigeuza hali mpya ya Vita Baridi kuja kuwa mzozo mkubwa wenye kuhusisha matumizi ya silaha duniani kati ya Urusi na mataifa ya magharibi.

Hakuna cha kufurahia

Mawaziri wa mambo ya nje wamekubaliana juu ya vikwazo hivyo vipya dhidi ya Urusi wakati wa mazungumzo ya dharura yaliyoitishwa baada ya watu kadhaa kuuwawa katika mapigano katika mji wa bandari wa Mariupol mashariki mwa Ukraine licha ya upinzani wa serikali mpya za sera kali za mrengo wa kushoto nchini Ugiriki.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amezungumza na waandishi wa habari mjini Brussels juu ya uamuzi wao huo. Amesema "Siwezi kusema kwamba nina furaha kwamba tumechukuwa uamuzi huu kwa sababu hali katika maeneo ya mzozo sio kitu cha kufurahiwa. Lakini kitu kimoja ambacho naweza kusema nakifurahia ni kwamba tumeweza kudumisha umoja wetu."

Federica Mogherini Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.
Federica Mogherini Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.Picha: AFP/Getty Images/B. Smialowski

Makubaliano hayo ya Umoja wa Ulaya yametanuwa vikwazo kadhaa vilivyowalenga watu na taasisi maalum ambavyo vimewahusisha zaidi ya watu 100 nchini Urusi na Ukraine kwa kuviongozea muda kwa miezi sita hadi hapo mwezi wa Septemba.Vikwazo hivyo viliwekwa baada ya Urusi kuinyakuwa Rasi ya Crimea kutoka Ukraine hapo mwezi wa Machi mwaka jana.

Vikwazo kutanuliwa

Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya pia wamekubaliana kongeza majina zaidi yatakayokumbwa na vikwazo vya marufuku ya safari na kuzuiliwa kwa mali zao katika kipindi kisichozidi wiki moja na kuanza kutafuta hatua nyengine zaidi inayofaa kuchukuliwa iwapo Urusi na waasi wataendelea kukiuka makubaliano ya amani yaliosainiwa Minsk hapo mwezi wa Septemba ambapo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakipuuzwa.

Waasi katika mji wa Mariupol mashariki mwa Ukraine .
Waasi katika mji wa Mariupol mashariki mwa Ukraine .Picha: Reuters

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki amesema ameikaribisha hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya na kuionya Urusi kwamba inatafakari kuiwekea nchi hiyo vikwazo vyake vyenyewe.

Psaki amekaririwa akisema ``Hii ni ishara tu zaidi kwamba vitendo vya siku chache na wiki zilizopita havikubaliki kabisa na kwamba kutachukuliwa hatua zaidi zitakazoileteya madhara nchi hiyo.”

Duru za kidiplomasia zinasema Urusi na Marekani zinajadili uwezekano wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kufanya ziara nchini Urusi kujadili mzozo huo wa Ukraine.

Imeelezwa kwamba mazungumzo ya kuandaa ziara hiyo yamekuwa yakifanyika kwa wiki kadhaa sasa na yumkini ziara hiyo ikafanyika siku au wiki chache zinazokuja.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Yusuf Saumu