UN:Dunia imepoteza dira kuhusu mabadiliko ya tabianchi
4 Desemba 2018Rais wa Nepal Bidhya Devi Bhandari amewaambia wajumbe wanaohudhuria mkutano wa kimataifa wa kujadili mabadiliko ya tabianchi nchini Poland COP24 kuwa nchi yake imekuwa ikikabiliwa na athari zisizostahili za mabadiliko ya hali ya hewa licha ya kuwa nchi hiyo haitoi kwa kiwango kikubwa gesi chafu ya Carbon.
Makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 mjini Paris, Ufaransa ya kupunguza kiwango cha joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili kwa kupunguza gesi chafu ya Carbon inayotoka hasa viwandani, yanahitaji mataifa tajiri kufadhili miradi ya kupunguza uchafuzi wa mazingira ya kima cha dola bilioni 100 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020 ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kuweza kufikia malengo ya kutumia nishati isiyochafua mazingira.
Lakini mataifa maskini yanalalamika kuwa nchi tajiri ambazo kwa sehemu kubwa ndiyo zinazotumia nishati zinazochafua mazingira kama makaa ya mawe, hazijachukua hatua za kutosha kuzisaidia kukabiliana na ongezeko la joto duniani.
Nchi tajiri zalaumiwa
Makubaliano yaliyofikiwa Paris yalipata pigo kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kujiondoa kutoka makubaliano hayo na kuna hofu kuwa hakuna utashi wa kisiasa kutoka pia mataifa mengine tajiri kushughulikia kitisho hicho cha mazingira, huku mazungumzo chungu nzima kuhusu tabia nchi yakijikokota.
Hakuna taifa hata moja la kundi la nchi ishirini zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi G20 iliyotuma wajumbe wa ngazi ya juu katika mkutano huo wa Umoja wa Mataifa wa COP24 ulioanza rasmi jana Jumatatu.
Ulimwengu hivi sasa unashuhudia majanga kama mafuriko, vimbunga, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, mikasa ya moto katika misitu na ukame mbaya.
Hapo jana, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyaonya mataifa karibu 200 yanayohudhuria mkutano huo wa COP24 kuwa mpango wao wa kujaribu kupunguza viwango vya joto duniani umepoteza njia akiongeza kuwa licha ya kushuhudia athari za mabadiliko ya tabia nchi kote duniani bado watu hawachukui hatua za kutosha wala kupiga hatua za haraka kuepusha majanga.
Ripoti kadhaa za Umoja wa Mataifa zimetahadharisha kuwa viwango vya gesi ya Carbon viko juu mno, rekodi ambayo haijashuhudiwa katika kipindi cha miaka milioni tatu huku miaka minne iliyopita ikitajwa kuwa yenye joto zaidi katika historia ya dunia.
Kundi la wanasayansi 90 huru mwezi Oktoba mwaka huu lilionya kuwa binadamu sharti wapunguze utoaji wa gesi chafu kutoka viwandani kwa hadi asilimia hamsini katika kipindi cha miaka 12 ijayo ili kuepuka kuongezeka zaidi kwa viwango vya joto ambavyo vitasababisha majanga makubwa mno duniani.
Mwandishi: Caro Robi/Afp/Ap
Mhariri: Iddi Ssessanga