UN yaitaka Taliban kuondoa sheria kandamizi kwa wanawake
27 Februari 2024Zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wameutaka utawala wa Taliban kuondoa sheria zote zinazokandamiza na kuwabagua wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku elimu ya wasichana na haki ya wanawake kufanya kazi na kutembea kwa uhuru.
Taarifa ya wajumbe 11 kati ya 15 wa baraza hilo la Umoja wa Mataifa imelaani ukandamizaji wa Taliban kwa wanawake na wasichana tangu walipoingia madarakani mnamo Agosti mwaka 2021.
soma pia: Taliban yakataa kushiriki mkutano kuhusu Afghanistan
Wajumbe hao pia wamehimiza ushiriki wa wanawake katika masuala mbalimbali ya umma, kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kijamii hasa katika ngazi ya kufanya maamuzi.
Wawakilishi wa mashirika ya kiraia ya Afghanistan, wakiwemo wanawake walishiriki katika mkutano huo uliofanyika mjini Doha, Qatar japo Taliban walikataa kuhudhuria.
Utawala wa Taliban haujatambuliwa na nchi yoyote huku mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Afghanistan akiwaonya viongozi hao kuwa, utawala huo kamwe hautatambuliwa kimataifa hadi watakapoondoa sheria zinazokandamiza na kuwabagua wanawake na wasichana.