Taliban yakataa kushiriki mkutano kuhusu Afghanistan
20 Februari 2024Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ofisi ya mambo ya nje inayoongozwa na Taliban ilikataa kuhudhuria mkutano huo wa Doha wakati Umoja wa Mataifa ulipokataa sharti la Taliban la kuhudhuria kama mwakilishi rasmi wa pekee wa Afghanistan.
Guterres amesema masharti ya aina hiyo hayakubaliki kwa sababu ni sawa na kuitambua Taliban kama serikali halali ya nchi hiyo. Amesema baada ya kukamilika kwa mkutano huo wa siku mbili kuwa ataanzisha mchakato wa kumteuwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa atakayeratibu ushirikiano kati ya utawala wa Taliban nchini Afghanistan na jamii ya kimataifa.
Serikali ya Taliban mjini Kabul haijatambuliwa rasmi na serikali yoyote nyingine tangu ilipochukua madaraka mwaka wa 2021, na kuweka tafsiri kali ya sheria za Kiislamu ambazo zimewawekea vikwazo wanawake kushiriki katika karibu kila sekta ya maisha ya umma.