1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya mzozo wa Yemen umeongezeka

Josephat Charo
17 Machi 2021

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa harakati za kijeshi zinazofanywa na waasi wa kundi la Houthi nchini Yemen zimeuchochea zaidi mzozo wa miaka sita katika taifa hilo maskini kabisa la kiarabu.

https://p.dw.com/p/3qiuh
Jemen Explosionen in Sanaa
Picha: Khaled Abdullah/REUTERS

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen, Martin Griffiths na Mkuu wa shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja huo Mark Lowcock wamelielezea baraza la usalama la Umoja wa Mataifa juu ya hali ya kisiasa, kiuchumi na kibinadamu ilivyo Yemen, ambayo inafanywa kuwa ngumu na hatua ya serikali kuzuia meli za mafuta kuingia bandari kuu ya Hodeida inayodhibitiwa na Wahouthi.

Griffiths amesema kundi la waasi wa Houthi linaendelea na harakati yake katika eneo lenye utajiri wa mafuta na gesi la Marib, ambalo ni ngome ya mwisho ya serikali na ambako shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM, linasema ni nyumbani kwa Wayemen takriban milioni moja waliolazimika kuyakimbia makazi yao. Operesheni ya Wahouthi Marib inaendelea kuwaweka katika hatari kubwa raia na vikosi vya pande zote zinazopigana vimepata hasara kubwa katika vita ambavyo havihitajiki.

Griffiths aidha amesema Wahouthi pia wanaendelea kuongeza mashambilizi kutumia ndege zisizo rubani na makombora nchini Saudi Arabia kuwalenga raia na miundombinu ya biashara. Amesema mashambulizi ya kulipiza kisasi kutokea angani kuelekea Sanaa yanahatarisha maisha ya raia wanaoishi mjini humo.

Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Martin Griffiths, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya YemenPicha: Getty Images/AFP/S. Stjernkvist

Mbali na kuzungumzia madhila wanayoyapitia raia wa Yemen, Griffiths pia amekumbusha juu ya hatma ya wahamiaji nchini Yemen na ametaka uchunguzi huru ufanyike kufuatia moto uliozuka Machi 7 katika kituo kinachoendeshwa na Wahouthi mjini Sanaa. Wahamiaji wapatao 43 kutoka Ethiopia waliuwawa na wengine 170 kujeruhiwa katika moto huo.

"Lazima pafanyike uchunguzi huru kubaini chanzo cha moto huo ambao sasa umegeuka kuwa jambo linalozungumziwa sana na umma. Watu wote nchini Yemen bila kujali utaifa wana haki ya kulindwa na wawe salama." Alisema Griffiths.

Kitisho cha njaa chawakabili raia wa Yemen

Mkuu wa shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa Mark Lowcock amesisitiza juu ya kitisho cha njaa kinachoendelea kuongezeka nchini Yemen huku uchumi wa nchi hiyo ukiwa umeporomoka. "Kuporomoka kwa uchumi ni sababu kubwa ya kuendelea na kutanuka kwa baa la njaa linaloweza kuwa kubwa. Kudorora kwa uchumi pia kunachochea hali ya kukosekana uthabiti kama ilivyodhihirishwa na maandamano ya hivi karibuni," alisema Lowcock.

Lowcock pia ametaka hatua zichukuliwe kuiimarisha sarafu ya Yemen, real, akisema hii ni mojawapo ya mambo mepesi ya kufanya kupunguza makali ya athari katika uchumi wa taifa hilo. Real ya Yemen imepoteza thamani kwa viwango vya kutisha katika miezi ya hivi karibuni.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema utawala wa rais Joe Biden wa Marekani umeaongeza juhudi za kidiplomasia kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuufikisha mwisho mgogoro wa Yemen. Hata hivyo ameonya hakuwezi kuwa na usitishaji mapigano na amani Yemen ikiwa Wahouthi wataendeleza mashambulizi yao ya kila siku dhidi ya raia wa Yemen, Saudi Arabia na mataifa mengine katika eneo hilo.

(afpe, ape)