1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yalaani shambulio la Houthi dhidi ya Saudi Arabia

9 Machi 2021

Marekani imelaani shambulio la waasi wa Houthi nchini Yemen dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudia Arabia na kusema waasi hao hawaoneshi kujitolea katika juhudi za amani zinazoongozwa na nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3qNJZ
US-Außenministerium Ned Price
Picha: Nicholas Kamm/AFP/AP/dpa/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price amesema kuwa kundi la waasi wa Houthi nchini Yemen lazima lioneshe kujitolea kwake kushiriki katika mchakato wa kisiasa wa kuafikia amani nchini humo baada ya kundi hilo kudai kuhusika katika mashambulio ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya Saudi Arabia.

Price ameongeza kuwa viongozi wa kundi hilo la waasi lenye mafungamano na Iran wanapaswa kukomesha mashambulio na kujihusisha na mazungumzo hii ikiwa njia ya pekee ya kupata ufanisi kwa sulushisho la kisiasa linalotafutwa. Price amesemamashambulio hayo hayakubaliki na kwamba yanahatarisha maisha ya raia wanaowajumuisha wale wanaotoka  Marekani.

Yemen Huthi Kämpfer
Wafuasi wa kundi la waasi wa Houthi nchini YemenPicha: Hani Mohammed/AP Photo/picture-alliance

Wakati huo huo, Ikulu ya White House imeelezea wasiwasi kuhusu vitisho vya kweli vya usalama kwa Saudi Arabia kutoka kwa kundi hilo la waasi na kwengineko katika kanda hiyo baada ya mashambulio hayo dhidi ya sekta ya mafuta nchini humo. Ikulu hiyo imesema kuwa itatafuta njia za kuboresha msaada wa ulinzi kwa Saudi Arabia.

Rais wa Marekani Joe Biden alikuwa ameweka kipaombele katika kumaliza mapigano ya miaka sita ambayo yamechangia katika kile ambacho Umoja wa Mataifa imekitaja kuwa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu kwa kumteuwa mjumbe Tim Lenderking kujaribu kusimamia juhudi za kutafuta amani nchini Yemen. Utawala wa Biden pia uliliondoa kundi hilo la waasi wa Houthi kutoka kwa orodha ya makundi ya ugaidi katika kujibu malalamiko kutoka kwa makundi ya msaada ambayo hatua za Marekani huweka operesheni zao katika hali ya hatari.

Kundi hilo la waasi wa Houthi limekuwa likikabiliana na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen kwa muda wa miaka sita sasa katika mzozo unaochukuliwa kama vita vya wakala kati ya Saudi Arabia na Iran.