1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa Monusco waondoka mjini Butembo

23 Agosti 2022

Baada ya karibu wiki 2 tangu kuzuka maandamano makubwa ya kutaka ujumbe wa kulinda amani wa Ukija wa Mataifa nchini Congo Monusco kuondoka huko Butembo, askari wa Ujumbe hatimaye wameondoka na kwenda mahala kwengine.

https://p.dw.com/p/4FuUR
Demokratische Republik Kongo | Proteste in Goma gegen UN Mission MONUSCO
Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Mashirika ya kiraia yanasema hatua hiyo  ni ushindi wa kwanza katika safari ya kuilazamisha Monusco kuondoka kikamilifu kwenye mkoa wote wa Kivu ya Kaskazini. Kuondoka Butembo kwa wafanyakazi wote wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa nchini Congo Monusco, kulipokelewa kwa shangwe na baadhi ya wakaazi wa mji huo wa kibiashara, walioandamana kwa zaidi ya wiki moja kuitaka tume hiyo kufungasha virago vyake.

Waandamanaji ambao wiki zilizopita waliwapoteza wenzao kadhaa waliopigwa  risasi, wanaishuku Monusco kutowajibika ipaswavyo, ilikukabiliana na makundi ya waasi na kubwa kuliko yote likiwa ni lile la kigaidi ADF, ambalo limeshawauwa maelfu ya wakaazi kwa kuwakata kwa mapanga katika eneo hili. Akizungumza na wanahabari katika mji wa Butembo, Meya wa mji huo kanali Roger Mowa aliwaomba wakaazi wa Butembo kuachana sasa na maandamano ilkuendesha shughuli zao za kawaida kwani Monusco haipo tena mjini humo.

"Monusco ambayo ilikuwa sababu ya vurugu nyingi imeondoka Butembo na tunaomba tukiwasihi raia kutulia pale tukifanya shughuli za kawaida nasio kuendelea na mifarakano isiyo na maana. Kwa kweli Monusco imeondoka, imeondoka Butembo," alisema Roger Mowa

Kwa upande wake, mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji wa Butembo Pasta Mathe Saanane, akiridhika na kuondoka Butembo kwa askari wa Umoja wa mataifa pamoja na wafanyakazi wake, ametangaza nia ya mashika yao kuitaka tume ya Monusco kuondoka katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini.

"Huu ni ushindi wa kwanza lakini tunataka iondoke katika wilaya ya Beni na pia wilaya ya Lubero. Na kwanini wasiuhame mkoa wote wa Kivu ya Kaskazini?" alisema Pasta Mathe Saanane.

Wapiganaji wa Maimai waushambulia mji wa Butembo 

Karte - Nord-Kivu, Demokratische Republik Kongo - DE
Ramani inayoonyesha ulipo mji wa Butembo DRC

Na wakati baadhi ya wakaazi wa Butembo wanashangilia kuondoka kwa Monusco katika mji wao, wapiganaji wa maimai nao waliushambulia mji huo alfajiri ya leo. Matokeo ya awali ya shambulizi hilo ni kuuawa kwa mpiganaji mmoja wa maimai na mwengine kutekwa nyara na wanajeshi wa serikali waliowafurusha wapiganaji wa maimai toka mji wa Butembo.

Mji wa Butembo ukiwa unakabiliana na changamoto chungu nzima za kiusalama,wadadisi wa masuala ya kiuasalama katika eneo hili wanahofia mashambulizi zaidi mnamo siku za usoni,viunga vya mji huo vikiwa vinayahifadhi kwa kiwango kikubwa makundi ya wapiganaji.

Na ili kukabiliana na mashambulizi zaidi,wadadisi hao wanaliomba jeshi kuvirundika  vikosi vyake pembezoni mwa Butembo. Tangu oktoba 2018, wilaya ya Beni inakabiliwa na mauwaji ya kukatwa kwa mapanga pamoja na risasi, mauwaji yanayofanywa na kundi la kigaidi kutoka Uganda ADF.

Vitendo vya kikatili vya kundi hilo vimeshawapelekea wakaazi wengi kuvihama vijiji vyao nakuishi maisha ya hohe hahe katika maeneo walikombilia. Wanachokiomba kwa serikali ya Congo ni kuwatokomeza ADF, jambo litakalo wapelekea kurudi katika mashamba yao nakuanzisha shughuli za kilomo ilikukidhi mahitaji yao.

Mwandishi: John Kanyunyu DW Beni