Ujerumani yazindua mkakati mpya wa kuamiliana na China
13 Julai 2023Ukilenga kuweka uwiano kati ya maslahi kinzani ya taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, waraka huo unaainisha mabadiliko makubwa katika msimamo wa Ujerumani kuelekea China kama mshirika, mshindani na mpinzani wa kimfumo.
Waraka huo wenye kurasa 64, ambao serikali inasema ni sehemu muhimu ya mkakati wa Umoja wa Ulaya kuelekea China, unalenga kuwa halisi lakini siyo ujinga, kulingana na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock. Waraka huo ni matokeo ya miezi kadhaa ya malumbambano ndani ya serikali ya Ujerumani kuhusiana na mkakati wake kuelekea China.
Wakati Baerbock, mwanasiasa kutoka chama mshirika katika serikali ya mseto cha Watetezi wa Mazingira, ameshinikiza msimamo mkali zaidi na msisitizo juu ya haki za binadamu, Kansela Olaf Scholz, Msosho Demokrat, ameunga mkono msimamo ambao ni rafiki zaidi kwa biashara.
Muungano wa Scholz wa vyama vitatu ulikuwa umeahidi baada ya kuingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2021, kuunda "mkakati mpaka wa China." Ujerumani ndiyo yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya na ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu katika umoja wa Ulaya.
Soma pia: Ujerumani, China zafanya mazungumzo ya ngazi ya juu
Mkakati wake unalenga kuweka usawa: Unataka kubakisha uhusiano mzuri na China, ambyo ndiyo mshirika wake mkubwa zaidi wa kibiashara katika miaka ya karibuni, licha ya wasiwasi kuhusiana na ubabe unaozidi wa China na kukataa kukosoa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Sera hiyo inaashiria usawa uliosawazishwa vizuri kati ya Baerbock na Scholz ndani ya muungano unaotawala, ambao ni matokeo ya kile Baerbock alichokiita "kutafuta maelewano... ambayo ndiyo msingi wa demokrasia.
Kupunguza hatari kunahitajika
Waraka huo wa kimkakati unabainisha kwamba "wakati utegemezi wa China kwa Ulaya unazidi kupungua, utegemezi wa Ujerumani kwa China umepata umuhimu mkubwa katika miaka ya hivi karibuni.
Serikali ya Ujerumani imesema haikukusudia kuzuwia ukuaji na maendeleo ya kiuchumi ya China, lakini wakati huo imeongeza kuwa kuondoa hatari kunahitajika haraka.
Soma pia: China yasema Beijing inapendelea ushirikiano na Ujerumani
Berlin inafuatilia kwa wasiwasi namna China inavyojitahidi kushawishi utaratibu wa kimataifa kulingana na maslahi ya mfumo wake wa chama kimoja na hivyo kupuuza misingi ya utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria, kama vile hadhi ya haki za binadamu.
Hata hivyo Ujerumani pia imeangazia uwezekano wa ushirikiano zaidi, ikibainisha kwa mfano kwamba "haitawezekana kushinda mzozo wa tabianchi bila China".
Ikiwa na kumbukumbu mbaya ya utegemezi wake kwa nishati ya gesi kutoka Urusi na kuumizwa na uvurugaji wa mifumo ya ugavi wakati wa janga la UVIKO-19, Ujerumani imekuwa ikiongeza juhudi za kuondokana na utegemezi wa China.
Chanzo: mashirika