1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yajiunga na vita dhidi ya uharamia Somalia

Thelma Mwadzaya19 Desemba 2008

Leo Ijumaa bunge la Ujerumani litaidhinisha kwa umbali gani wanamaji wa Ujerumani wataruhusiwa kushiriki katika operesheni ya Umoja wa Ulaya kupambana na maharamia wenye silaha za kisasa na waliojiandaa vizuri.

https://p.dw.com/p/GJfH
Ramani ya SomaliaPicha: AP



Mashambulizi ya maharamia katika Pembe ya Afrika sasa yamefikia kiwango cha kuwa kitisho kikubwa duniani.Vitendo vyao haramu vimekuwa njia ya kujipatia vitita vya fedha katika Pembe ya Afrika.


Hivi sasa mabaharia 250 na zaidi ya meli 12 wametekwa nyara na maharamia wa Kisomali.Mwaka huu peke yake kumefanywa mashambulizi 92 katika Pembe ya Afrika.Hiyo ni kwa mujibu wa Ofisi ya Kimataifa ya Misafara ya Meli IMB iliyo na makao yake London Uingereza.Kwa wastani, pesa zinazodaiwa kuikomboa kila meli moja ni kati ya dola milioni moja hadi mbili.Lakini kwa meli kubwa ya Saudi Arabia "Sirius Star" iliyobeba mafuta, maharamia wamevunja rekodi kwa kutaka dola milioni 25.Kwa mujibu wa vyombo vya habari katika kanda hiyo,fedha za kukomboa meli,kawaida hupelekwa katika meli yenyewe.Lakini mbali na maharamia nani anaenufaika kutokana na vitita hivyo vya pesa?

Mtaalamu wa masuala ya Somalia,Roger Middleton anaamini kuwa idadi kubwa ya maharamia wanashirikiana na makundi ya wahalifu katika nchi za ngámbo.Alipozungumza kutoka ofisi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa mjini London alisema "Wengi wao wanafuata maslahi yao na huteka nyara meli yo yote inayopita njia-lakini ni hakika kuwa makundi hayo ya maharamia yanashirikiana na wengine katika nchi za nje.Maharamia wengine husema waziwazi kuwa wana washirika wao katika Mashariki ya Kati,Ulaya na Marekani."


Bila shaka uharamia ni matokeo ya kukosekana serikali inayofanya kazi nchini Somalia.Tangu mwaka 1991 hakuna serikali wala sheria zinazofanya kazi nchini humo.Serikali dhaifu ya mpito inayoongozwa na Rais Abdullahi Yusuf Ahmed kwa mara ya kumi na tano inajaribu kupata suluhisho la amani nchini Somalia.Kwa mujibu wa mashirika yanayotoa misaada ya kiutu,nusu ya Wasomali wanategemea misaada kutoka nchi za kigeni na miongoni mwao maelfu wanateseka kwa njaa.Umasikini mkubwa,biashara ya magendo inayoshamiri na maafisa wanaohusika na rushwa serikalini ni mambo yanayowapa maharamia nafasi nzuri kuitumia kanda hiyo kufanya vitendo vyao vya uhalifu.

Kwa maoni ya Middleton,vitendo vya uharamia katika Pembe ya Afrika vinavyousumbua ulimwengu mzima ni matokeo ya kutokuwepo serikali inayofanya kazi nchini Somalia.Na hali hiyo imesababishwa na mambo mengi.Sababu mojawapo ni jumuiya ya kimataifa kutotia sana maanani matatizo ya Somalia.Ikiwa kweli tunataka kukomesha uharamia basi matatizo ya kisiasa nchini Somalia yanapaswa kupatiwa ufumbuzi.Hiyo ni njia pekee ya kupata suluhisho la kudumu.