Uharamia uliochacha katika pwani ya Somalia unazidi kuzusha hofu miongoni mwa makampuni yanayosafiri kupitia eneo hilo.
30 Mei 2008Kufuatia kuongezeka kwa visa hivyo vya utekaji nyara Meli shirika la kimataifa la safari za baharini limeyatolea mwito makampuni yote ya meli zinazosafiri kupitia pwani hiyo ya Somalia kuwa waangalifu.
Meli za Mv Arean na Mv Lehmann Timber zilitekwa nyara katika ghuba ya Aden jumatano katribu na mahala ambako meli nyingine ilitekwa nyara mwishoni mwa wiki.Hayo yamethibitsihwa na afisa mmoja wa kenya anayehusika na safari za baharini bwana Andrew Mwangura.
Afisa huyo amesema maharamia wakisomalia walizivamia meli hizo mbili na kuziteka nyara lakini hadi sasa hawajatoa mapendekezo yoyote kuhusu kuiachilia meli hiyo.Aidha amefahamisha kwamba hadi sasa hawajapata taarifa zozote kuhusiana na waliokuwa ndani ya meli hizo,mahala zilikotokea na wapi zilikokuwa zinakwenda.
Hata hivyo ameeleza kwamba Meli ya Mv Arean iliyokuwa na bendera ya Uturuki inamilikiwa na kampuni ya Arkia kutoka kisiwa cha Malta lakini hakuna habari zilizotolewa kuhusiana na meli ya Mv Lehman.
Jumapili iliyopita maharamia wakisomali pia waliiteka nyara meli ya Uholanzi ya MV Amiya ikiwa na wafanyikazi tisa raia wa Urussi na Ufilipino katika eneo hilo hilo ambalo limekuwa hatari kwa meli zinazopitia pwani ya Somalia.
Katika miaka ya hivi karibuni eneo hilo limezidi kuwa hatari ambapo pia meli za kusafirisha misaada kwa wasomali wenyewe zinatekwa nyara kama anavyokumbusha bwana Inaya Sikudrati mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya safari za meli ya Motaku kutoka Mombasa.
Shirika la kimataifa linalohusika na safari za baharini pia limezungumzia hatari iliyopo katika pwani ya Somalia na kuzitolea mwito kampuni zote za usafiri wa baharini kuchukua tahadhari kubwa wanapopitia eneo hilo.
Shirika hilo limesema kwamba maharamia wakisomali wanatumia silaha kali kali pamoja na maguruneti wakati wanapojaribu kuvamia meli na kuiteka nyara.
Bwana Inaya Sikudrata mkurugenzi wa kampuni inayosafirisha zaidi misaada ya kimataifa nchini Somalia anasema hatari iliyopo Sasa inabidi meli zisindikizwe na vikosi vya usalama.
Ni hali kama hiyo ambayo pia imezifanya nchi za Ufaransa na Marekani kutia msukumo katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa kupitisha azimio ambalo litaziruhusu nchi kutuma manuwari za kivita katika pwani hiyo ya Somalia kukabiliana na uharamia huo.
Kimsingi kikwazo dhidi ya Somalia kuingiza sialaha kilichowekwa mwaka 1992 na Umoja wa Mataiafa kinazuia manuawari za kivita za kigeni kuingia katika bahari ya Somalia ingawa kuna baadhi ya nchi zimekiuka amri hiyo.Aidha wanamgambo wakisomali wameapa kuanzisha tena mapambano dhidi ya maharamia ambao shughuli zao zinazidi kutatiza safari za baharini ikiwa ni pamoja na kusafirisha misaada nchini humo.
Mwezi April vikosi vya eneo lililojitenga na Somalia la Puntland waliikomboa meli moja iliyokuwa imetekwa nyara kutoka umoja wa falme za kiarabu ambapo mmoja wa maharamia hao aliuwawa na wengine saba wakakamatwa na baadae kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Lakini mwezi huohuo maharamia waliiliteka nyara boti la kifahari la Ufaransa likiwa na wafanyikazi wake 30 na baadae boti jingine la uhispania.Maboti yote mawili yaliachiliwa huru baada ya kuzuiliwa wiki kadhaa na fedha chungunzima zikapewa maharamia hao kabla ya kuacha huru maboti hayo.