Ujerumani yaandaa kongamano kuhusu Libya
23 Juni 2021Mkutano huo unaofanyika leo kwenye ofisi za mambo ya nje ya Ujerumani mjini Berlin, unawakutanisha mawaziri wa masuala ya kigeni, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken.
Mkutano wa leo unafuatia ule uliofanyika Januari mwaka 2020 na kuwakutanisha viongozi ambao walikubaliana kuheshimu marufuku ya silaha na kuzishinikiza pande zinazohasimiana nchini Libya kufikia makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano.
Soma zaidi: UN yataka wanajeshi wa kigeni na mamluki kuondolewa Libya
Ujerumani imekuwa ikijaribu kuwa mpatanishi mkuu katika mzozo huo, huku nchi zinazohusika kwenye mchakato huo zikiwa ni pamoja na Marekani, China, Urusi, Uingereza, Ufaransa ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, sambamba na Italia, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu. Serikali ya mpito ya Libya pia imekuwa ikishiriki katika mchakato huo.
Kabla ya mkutano wa leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas alisema, hatua kubwa imepigwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. "Baada ya kufikiwa kwa maendeleo kadhaa katika miezi michache iliyopita, tuna matumaini na ndiyo sababu tunaamini ni busara kuwaalika wale wote waliohusika kwenye mkutano wa kwanza kuhusu Libya katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje kwa mara nyingine tena, ili kuhakikisha njia sahihi inachukuliwa kuelekea Libya na kuona uchaguzi ukifanyika na kwamba hakuna tena vikosi vya kigeni nchini Libya katika siku zijazo." Amesema Maas.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Oktoba mwaka uliopita yanayosisitiza kuondoka kwa wapiganaji wa kigeni na mamluki ndani ya siku 90, yamesababisha kufikiwa kwa mkataba wa kuandalaiwa kwa uchaguzi ambao umepangwa kufanyika Desemba 24 pamoja na kuundwa kwa serikali ya mpito ambayo ilichukua madaraka mwezi Februari.
Hata hivyo, Maas ambaye jana alikutana na waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Libya na waziri wa mambo ya nje, amesema bado kuna changamoto nyingi zinazoikabili Libya. Maas amesema mkutano wa leo utazindua awamu mpya, ambapo hawatoizungumzia tu Libya, lakini wanazungumza na Walibya wenyewe kuhusu mustakabali wa nchi yao.
Soma zaidi: Wapiganaji 78 wa Kamanda Haftar waachiliwa huru Lipya
Mjumbe maalum wa Marekani nchini Libya, Richard Norland ameipongeza hatua ya Walibya kushirikishwa katika mazungumzo hayo.
Asubuhi hii, Maas amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken mjini Berlin kabla ya kuanza kwa mkutano wa Libya. Blinken atakutana pia na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na baadae ataizuru Ufaransa, Italia na Vatican.
DPA,reuters,AP,AFP