Ujerumani kusaidia kubaini visa vya Mpox nchini Kongo
21 Agosti 2024Wizara ya ushirikiano wa kimaendeleo ya Ujerumani imetangaza hatua ya kupeleka maabara inayohamishika nchini Kongo, na kuongeza kuwa kuna mipango pia ya kutoa mafunzo kwa wataalamu zaidi ili waweze kutambua dalili na kuwafahamisha watu kuhusu hatua za kuzuwia ugonjwa huo. Kwa mujibu wa wizara hiyo, hatua sawa na mafunzo hayo zilichukuliwa mashariki mwa Kongo mwezi Juni. Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze amesema serikali za Afrika zimeiomba msaada jumuiya ya kimataifa, na kwamba misaada hiyo inapaswa kutolewa.
Kwengineko, shirika la Afya duniani, WHO limetangaza tahadhari ya hali ya juu kabisaa kutokana na milipuko ya mpox barani Afrika, na aina mpya ya kirusi hicho ambayo inaweza kuwa hatari zaidi. Thailand imeripoti hii leo kisa cha kwanza kinachoshukiwa cha aina hiyo hatari ya mpox, kutoka kwa mgonjwa aliyewasili mjini Bangkok Agosti 14.
Visa vya mpox vyaongezeka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Vipimo vya maabara vilikuwa vinafanyika kuthibitisha iwapo ni aina hiyo hatari inayojulikana kama clad1b, lakini maafisa wamesema wanaamini ni kutoka aina ya kwanza ya clad1. Mkuu wa kitengo cha udhibiti wa magonjwa nchini humo, Thongchai Keeratihattayakorn amesema mwathirika huyo, raia wa Ulaya mwenye umri wa miaka 66, ambaye alisafiri kutoka nchi ya Afrika, amewekwa kwenye karantini.
Thongchai ameuambia mkutano wa waandishi habari kuwa maafisa wa afya wanawafuatilia watu 42 waliotangamana na mgonjwa huyo. Nako nchini Argentina, mamlaka zimeripoti kuizuwia meli ya mizigo katika Mto Panama, kuhusiana na kisa kinachoshukiwa kuwa cha mpox ndani ya meli hiyo. Meli hiyo inayopeperusha bendera ya Liberia ilikuwa inasafiri kutoka Santos, Brazil, kuchukua mzigo kulingana na wizara ya afya na chama cha wafanyabiashara nchini Argetina.
Hali inazidi kuwa mbaya barani Afrika
Visa vya mpox na vifo vinaongezeka barani Afrika, ambako milipuko imeripotiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda tangu mwezi Julai. Ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vinavyoambukizwa kutoka kwa wanyama, lakini unaoambukiza kutoka binadamu kwenda binadamu mwingine kupitia kutangamana kimwili, unasababisha homa, maumivu ya misuli na mapele makubwa.
Ulaya kuzalisha chanjo zaidi za ugonjwa wa homa ya nyani
Wakati mpox inajulikana kwa miongo kadhaa, aina mpya ya kirusi chake kinachoambukiza kwa kasi, cha Clade 1b, imesabisha ongezeko la karibuni zaidi katika visa. Ugonjwa huo ambao zamani ulijulikana kama monkeypox, uligundulika nchini Denmark mwaka 1958 katika nyani waliokuwa wanahifadhiwa kwa ajili ya utafiti.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeripoti zaidi ya visa 16,000 na vifo 500 mwaka huu. na Mnamo Agosti 15, Sweden iliripoti kisa cha kwanza cha kirusi aina ya Clade 1 nje ya bara la Afrika.
Chanzo: dpa/afp