Ufaransa yaitaka Mali kuzungumza na waasi
30 Januari 2013Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, Philippe Lalliot, amesema hivi leo kwamba serikali ya mpito ya Mali lazima ianze mazungumzo ya haraka na jamii ya watu wa kaskazini, yakiwemo makundi yenye silaha yanayoitambua serikali hiyo.
"Serikali ya Mali lazima isicheleweshe mazungumzo na wawakilishi halali wa watu wa kaskazin na makundi yasiyo ya kigaidi lakini yenye silaha. Ni majadiliano baina ya kusini na kaskazini tu, ndiyo yanayoweza kurudisha mamlaka kamili ya Mali kwenye eneo la kaskazini." Amesema Lallito alipokuwa akizungumza na shirika la habari la Reuters mjini Paris.
Lalliot alikuwa akizungumza baada ya wanajeshi wa Ufaransa kuingia kwenye mji wa Kidal, unaoaminika kuwa ngome ya mwisho kubwa ya waasi, hatua inayoashiria kuanza kwa awamu mpya kwenye operesheni ya wiki tatu ya kijeshi dhidi ya waasi wa Ansar Dine wenye mafungamano na al-Qaida.
Rais Traore atangaza tarehe ya uchaguzi
Kwa upande wake, Rais Dioncounda Traore wa Mali ametangaza hivi leo kwamba serikali yake itaitisha uchaguzi huru na wa haki tarehe 31 Julai, ikiwa ni kuakisi matakwa ya mataifa ya Magharibi yanayounga mkono mapambano yake dhidi ya waasi.
Msemaji wa Vuguvugu la Ukombozi wa Azzawad (MNLA) Mouusa Ag Assarid, amesema kwamba wako tayari kwa mazungumzo na serikali ya Mali kwa ajili ya kutafuta suluhisho la kisiasa.
Ag Assarid ameliambia shirika la habari la AFP akiwa mjini Paris, Ufaransa: "Tunataka mamlaka ya kujitawala na kujiamulia mambo yetu, lakini hayo yote yatatokana na makubaliano yatakayoamua kwa kiwango gani pande hizi mbili zinaweza kuafikiana."
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo ya eneo la Sahel, wanasema kwamba kufikiwa muafaka wa kisiasa baina ya serikali ya Mali na waasi linaweza kuwa jambo gumu sana.
Mshauri maalum wa Wakfu wa Utafiti mjini Paris, Francois Heisbourg, anasema kwamba "kuwafanya watu wa jamii ya Tuareg kupatana na raia wenzao wa Mali si rahisi, kwani baadhi ya makundi yalichukua uamuzi usio sahihi tangu mwanzoni."
Waasi wa jamii ya Tuareg wanaounganishwa na MNLA walianzisha uasi mwanzoni mwa mwaka jana, wakifanikiwa kuchukua haraka udhibiti wa eneo lote la kaskazini baada ya mapinduzi ya kijeshi mjini Bamako hapo mwezi Machi.
Hata hivyo, baadaye ushindi huo ulitekwa nyara na wapiganaji wa Kiislamu waliyoshirikiana nayo, ambao walitumia fursa hiyo kuanzisha utawala wao kwenye eneo hilo wanaloliita Azzawad.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf