Ubepari umeungusha ulimwengu wakati huu wa corona
5 Oktoba 2020Papa Francis aliielezea barua yake hiyo katika hotuba aliyoitoa katika uwanja wa St Peters mjini Roma jana Jumapili akiweka maono ya dunia baada ya virusi vya corona.
Barua hiyo ya maaskofu iliyopewa jina "Fratelli Tutti'' yani sote ni ndugu, imetoa wito wa kuwa na utu zaidi na mshikamano kutatua masuala kama mabadiliko ya tabia nchi na udhalimu unaotokana na ukosefu wa usawa wa kiuchumi.
Barua hiyo ya Papa ni moja ya mawasiliano muhimu anayoyatoa na yanatumika kama msingi wa mafundisho ya kikatoliki kwa kuchukua misimamo katika masuala fulani.
Kiongozi huyo wa kanisa katoliki pia amekosoa nadharia za mfumo wa kibepari akisema kuondokana na mifumo hiyo kutafungua njia ya kutatua matatizo ya kijamii.
Papa amesema udhaifu wa mifumo ya dunia hasa wakati huu wa janga la Corona umeonesha kuwa sio kila kitu kinaweza kutatuliwa kwa kuwa na uhuru wa masoko.
"Ni muhimu kuwa na sera nzuri za kiuchumi zinazoelekezwa katika kuinua au kuimarisha uchumi utakaowashirikisha wote, kuwa na ubunifu katika biashara na kuwezesha ukuaji zaidi wa ajira na sio ukosefu wa ajira," alisema Papa.
Amerejelea pia miito yake ya awali juu ya wale walio na utajiri mkubwa kuliko wengine, kuutumia kwa manufaa ya watu wote. Papa Francis ameongeza kuwa anatumai janga la Corona linaloikumba dunia kwa sasa na lililosababisha vifo vya zaidi ya watu milioni moja duniani, litahamasisha kuangaliwa tena kwa vipaumbele vya dunia.
"Pindi tu baada ya janga hili kumalizika itakuwa vibaya zaidi iwapo tutajikita katika ulafi au upendeleo na mifumo mipya ya kujilinda bila kujali wengine," aliongeza kusema kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani Papa Francis.
Papa ametaka uwepo wa undugu wa kidunia, watu na mataifa na pia kuwa na siasa nzuri zinazojenga.
(AP, dpa, Reuters) DW Page
/dw/en/pope-says-capitalism-failed-humanity-during-coronavirus-pandemic/a-55153004