Trump azindua mpango wa amani, Mashariki ya Kati
29 Januari 2020Rais Trump ameuzindua mpango huo uliosubiriwa kwa muda mrefu, sanjari na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kiongozi wa upinzani Benny Gantz, katika ikulu ya White House.
Trump amesema kwa pamoja wanaweza kuanza upya katika eneo la Mashariki ya Kati, na kusema ulikuwa ni mpango mgumu zaidi kuwahi kufikiwa. Amezishukuru serikali za Oman, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa msaada walioutoa wa kufanikisha mchakato wake.
Netanyahu ameiita siku ya jana kuwa ni ya kihistoria, akiifananisha na Mei 14, 1948, ambapo rais wa Marekani Harry Truman alikuwa kiongozi wa kwanza wa kimataifa kulitambua taifa la Israel.
Trump ameuita mpango huo kuwa ni suluhisho la kweli la mataifa mawili. Chini ya mpango uliopendekezwa, Jerusalem itasalia mji mkuu ambao hautagawanywa. Hata hivyo alisema mji mkuu wa taifa la Palestina katika siku za usoni utapaswa kuundwa na sehemu za Mashariki ya Jerusalem kupitia aina fulani ya makubaliano ya mipaka, yaliyofanana na maelezo ya maafisa wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, kabla ya kuzinduliwa kwa mpango huo.
Mpango huo pia unatoa muda wa miaka isiyozidi minne kwa Israel kusitisha ujenzi wa makaazi, ingawa utaruhusu taifa hilo kuendeleza udhibiti wa makaazi mengi ya Walowezi ambayo tayari imeyajenga.
Mpango huo ambao umecheleweshwa kwa miaka miwili, tayari umepingwa na Wapalestina, ambao hata hivyo wawakilishi wake hawakualikwa kwenye mkutano huo wa uzinduzi. Maafisa wa Palestina wanadai kwamba Trump anaipendelea zaidi serikali ya Isreal na anayetafuta kuiimarisha serikali hiyo ya Netanyahu.
Kumekuwepo na maoni tofauti baada ya kutangazwa kwa mpango huo. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema kwenye taarifa yake kwamba wanaikaribisha hatua hiyo na kuahidi kuifuatilia kwa karibu. Hata hivyo amesema suluhu ya mataifa mawili na inayokubalika na pande zote ndio pekee inayoweza kuleta amani ya kudumu kati ya Israel na Palestina.
Hapo jana, maelfu ya Wapalestina waliandamana kwenye mitaa ya Gaza kuupinga mpango huo huku wakizichoma moto picha za Trump na Netanyahu. Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh, ambaye ni mpinzani wa rais wa Palestina Mahmoud Abbas amemtaka rais huyo kuahidi kuwaunga mkono kikamilifu katika kuukataa mpango huo.
Rais Abbas aliyeshiriki mazungumzo ya awali na Israel chini ya usimamizi wa Marekani lakini akijitenga na mpango huo wa Trump amenukuliwa akisema mpango huo aliouita kuwa ni "njama" hautapita, huku akiahidi kuupinga kwa namna yoyote baada ya kukutana na pande tofauti za Palestina katika mji wa Ramallah.
Mwanadiplomasia wa juu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel amesema wanausoma mpango huo na kuufuatilia, huku Uingereza inayoondoka kwenye Umoja huo siku ya Ijumaa, ikiukaribisha kwa bashasha, sawa sawa na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kupitia msemaji wake Stephane Dujarric amesema wataendeleza msimamo wao kuhusu suluhisho la mataifa mawili kwa kuzingatia mipaka iliyowekwa kabla ya vita vya mwaka 1967, wakati Israel ilipozinyakua Ukingo wa Magharibi na Gaza.
Urusi imesema itaupitia mpango huo na hatimaye kuzitolea mwito Israel na Palestina kuzungumza ana kwa ana ili kufikia makubaliano yatakayokubaliwa na pande zote, huku Uturuki ikiulaani vikali mpango huo, sawa sawa na Iran ambayo imesema ni kitisho kwa ustahmilivu wa kikanda. Vuguvugu la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran limesema ni mpango unaolenga kuwapokonya Wapalestina haki zao.