1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani inaamini suluhisho la mataifa mawili

Sylvia Mwehozi
27 Machi 2018

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas, amesisitiza msimamo wa Ujerumani katika suluhisho la mataifa mawili kwenye mzozo wa Israel na Palestina, huku akiwatolea wito Wapalestina "kutovunja madaraja".

https://p.dw.com/p/2v3aC
Westjordanland Heiko Maas trifft Mahmoud Abbas
Picha: picture-alliance/dpa7Zumapress

Maas, alitoa kauli hiyo siku ya Jumatatu baada ya mkutano wake na Ris Mahmoud Abbas a Palestina na Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina katika mji wa Ramallah kwenye Ukingo wa Magharibi. Aliwahimiza Wapalestina kufikiria kuijumuisha Marekani katika mchakato wa baadae wa majadiliano ya amani, akisisitiza kwamba juhudi za amani bila ya Marekani "zitakuwa ngumu".

Abbas aliikataa Marekani akisema si mpatanishi wa kuaminika kwa mzozo huo wa Mashariki ya Kati, baada ya Rais Donald Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel mnamo mwezi Desemba. Wapalestina wanadai Jerusalem Mashariki kuwa mji mkuu wa taifa la baadaye la Palestina.

"Katika hali hii ngumu, ninataka kuwahimiza watu hapa wasivunje madaraja", alisema Maas katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Palestina, Riyad al-Maliki.

"Serikali ya Ujerumani siku zote imekuwa na msimamo kwenye suluhisho la mataifa mawili na hilo halitabadilika," alisema Maas akiongeza kwamba anatambua haijakuwa rahisi.

Maas aahidi ushirikiano na Israel

Israel Jerusalem Heiko Maas trifft Benjamin  Netanjahu
Heiko Maas na waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Imago/photothek/X. Heinl

Al-Maliki aliwaambia waandishi wa habari kwamba Palestina pia inaunga mkono suluhisho la mataifa mawili na kwamba ina dhamira ya mazungumzo ya moja kwa moja na Israel na vita dhidi ya ugaidi.

"Tunategemea jukumu la Ujerumani katika Umoja wa Ulaya na jukumu la Umoja wa Ulaya katika mchakato wa amani," alisema.

Baadaye siku ya Jumatatu wakati wa mkutano wake na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem, Maas alisema msimamo wa Ujerumani siku zote umekuwa upande wa Israel.

"Ninaamini kwamba tunakubaliana karibu malengo yote", akibainisha hata hivyo kwamba kulikuwa na tofauti ya maoni wakati linapokuja suala la ufumbuzi wa mataifa mawili na makubaliano ya nyuklia na Iran, mshindani wa Israel kikanda. Israel inaukataa mkataba huo wakati Ujerumani ikiutetea.

"Katika urafiki kama huu, inawezekana kuzungumzia mambo ambayo hatukabiliani", alisema Maas.

Mahusiano ya Israel na Ujerumani

Israel Besuch Außenminister Maas in Yad Vashem
Maas akiweka shada la maua katika kumbukumbu ya wahanga wa mauaji ya HolocaustPicha: picture-alliance/dpa/I. Yefimovich

Suala la kuboresha mahusiano ya mataifa hayo imekuwa ajenda muhimu ya Maas tangu achukuwe majukumu yake mapya kama mwanadipolamsia wa juu wa Ujerumani. Wakati wa hafla ya kukabidhiana ofisi ya wizara ya mambo ya nje mjini Berlin, ambako alichukua mikoba ya Sigmar Bariel, Maas alisisitiza kwamba ilikuwa ni kwa sababu ya "Auschwitz kwamba niliweza kuchagua kuingia katika siasa".

Amerejea maneno yake siku ya jumatatu wakati alipokutana na manusura 30 wa mauaji ya Holocaust mjini Jerusalem.

Ziara ya siku mbili ya waziri huyo wa nje wa Ujerumani nchini Israel inakuja wakati muhimu katika mahusiano ya Israel na Ujerumani. Tangu uamuzi wa Kansela Angela Merkel wa kusitisha mazungumzo ya kila mwaka na Israel mapema mwaka uliopita, mahusiano baina ya nchi hizo mbili yalizidi kuzorota.

Merkel alijitetea kwa kusitisha mazungumzo hayo akisema alihitaji muda zaidi katika uchaguzi wa mwaka jana, ingawa ripoti kadhaa zilizofuatia ziliashiria kuwa uamuzi wa Merkel ulihamasishwa na kuendelea kwa ujenzi wa makazi katika ukingo wa magharibi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DW

Mhariri: Mohammed Khelef