TCRA:Hatujazuia vituo vya nje kurusha matangazo Tanzania
11 Agosti 2020Katika taarifa yake kwa umma, TCRA imesema ina dhamana ya kusimamia Sekta ya Utangazaji pamoja na Sekta nyingine za Mawasiliano, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa vituo vya Utangazaji vinazingatia weledi wa vipindi na habari au matukio yanayorushwa na vituo vyao.
TCRA imeongeza kwamba inatumia Kanuni zinazosimamia Sekta pamoja na kutoa leseni zilizo na masharti ya jinsi ya kutoa huduma za Utangazaji nchini.
Ili kuweza kusimamia vizuri maudhui ya nje yanayorushwa mubashara, Kanuni ya 37 ilifanyiwa marekebisho mwaka 2020 kwa kuongeza kanuni ndogo (2) inayokitaka Kituo chochote cha Utangazaji kinachotaka kujiunga na kituo kingine cha ndani au nje ya nchi kwa ajili ya kurusha matangazo yake yakiwemo yale ya mubashara kupata kibali/ruhusa ya kufanya hivyo kutoka TCRA, imesema taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imeongeza kwamba marekebisho hayo yanavihusu vituo vyote vya utangazaji vya Redio na Televisheni na watoa huduma za Maudhui Mtandaoni.
Kulingana na taarifa ya Mkurugenzi wa TCRA, Mamlaka hiyo inavielekeza vituo vya Utangazaji vinavyohitaji kurusha matangazo ya vituo vya Utangazaji vilivyoko nje ya nchi kuwasilisha makubaliano yao TCRA na kupata kibali kama utaratibu wa kawaida wenye lengo la kuleta ufanisi katika usimamizi wa maudhui yanayorushwa na vituo hivyo.
Kwa vituo ambavyo tayari vinarusha matangazo ya vituo hivi, vinatakiwa kuomba kibali/ruhusa husika na kuwasilisha makubaliano yao TCRA na sio kusimamisha matangazo au makubaliano yaliyopo. TCRA imevitaka vituo vyote kuwasilisha maombi yao ndani ya siku saba (7) tokea kutolewa kwa taarifa hii.
Akizungumza na DW kwa njia ya simu, Mkuu wa Kitengo cha Leseni za Mawasiliano TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka amesema kuwa;
"Hakuna redio ambayo tumepata ripoti yoyote iliyosimamisha, kwamba kanuni zilipotoka wengine walikuwa hawaelewi vizuri lakini wameelimishwa kwamba kinachotakiwa ni kuleta makubaliano yale kati ya redio ya hapa nchini na ile ambayo inarusha matangazo yake"
Mabadiliko haya yameibua mjadala mkubwa nchini Tanzania kwa sasa huku wadau wa habari na waandishi wa habari wakiwa na mitazamo tofauti juu ya mabadiloko haya.