Vyombo vya habari vya kimataifa mtegoni nchini Tanzania.
10 Agosti 2020Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya mawasiliano nchini humo imeifanya marekebisho ya kikanuni kwenye Kanuni zake za Maudhui ya Redio na Televisheni za mwaka 2020 ambapo kwa sasa itakuwa ni marufuku kwa Redio ama Televisheni kurusha maudhui kutoka kwenye vyombo vya habari ama mashirika ya habari kutoka nje.
Kanuni hizo zimewasilishwa hii leo na Mamlaka hiyo wakati wa kikao chake na wakuu wa vyombo vya habari vya kielekroniki kutoka Kanda ya Ziwa pamoja na waandishi wa habari kilichofanyika jijini Mwanza.
Meneja wa Mamlaka hiyo kwa kanda ya Ziwa Mhandishi Francis Mihayo ambaye ndiyo aliwasilisha mabadiliko hayo amesema kuwa kumefanyika maboresho kwa kuongeza kanuni ndogo ya sheria katika kifungu cha sheria namba 14 ya mwaka 202 " Yamefanyika marekebisho madogo, kwa kuzingatia sheria ndogo(1)(d) ambapo kwa sasa kila mwenye leseni ya Redio na Televisheni nchini hataruhusiwa kurusha maudhui kutoka vyombo vya nje bila kuwa na kibali kutoka TCRA,” amesema mhandishi Mihayo.
Mtihani mgumu kwa vyombo vya habari vya ndani ya Tanzania.
Mbali na Katazo hilo la kjiunga na vyombo kutoka nje,mabadiliko haya ya Kanuni pia yamevibebesha mzigo vyombo vya habari vya ndani kwa kuwajibika pale maudhui kutoka vyombo vya habari vya nje pamoja na mashirika ya habari yanapoonekana kukiuka sheria za nchi. "Pamoja na chombo kuwa na nafasi ya kupewa kibali cha kurusha maudhui hayo,pindi maudhui hayo yatakapokiukwa sheria ya nchi,TCRA haitashughulika na chombo kutoka nje bali chombo kilichorusha kitalazimika kubeba mzigo wa adhabu ambapo yaweza kuwa ni onyo,kufuta maudhui hayo ama faini”ameongeza Mhandishi Mihayo,
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, mwenye maudhui hataruhusiwa kutembea au kufanya biashara na raia wa kigeni inayohusiana na urushaji wa maudhui bila kuambatana na afisa wa serikali au mfanyakazi kutoka mamlaka.
Wadau wataka mamlaka kuwashirikisha wadau kabla ya maamuzi
Mabadiliko haya yamepokelea kwa hisia tofauti na waandishi wa habari pamoja na wakuu wa vyombo vya habari,ambapo baadhi yao wameitaka mamlaka hiyo kuangalia upya uamuzi wao. "Nadhani Mamlaka ingekaa kwanza na walengwa ili kujadiliana kuhusu mabadiliko haya kuliko kufanya maamuzi na kutuita kutusomea,hili siyo jambo jema.” Amesema Bernard James mtangazaji wa televisheni ya Star iliyopo jijini Mwanza.
Nao baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu na waandishi wa habari wamekosoa maudhui hayo kuwa yanakwenda kukiuka haki ya kupata taarifa pamoja na ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania. "Hatutakubaliana na mabadiliko haya kwa sababu ni mwendelezo wa kile tunachokipigia kelele kila siku kuwa tumekuwa na sheria na kanuni zinazobinya uhuru wa habari na vyombo vya habari” amesema Soko.
Soma zaidi:Tanzania yakanusha kukandamiza uhuru wa habari
Baadhi ya mashirika ya habari ya Kimataifa yanayorusha maudhui kwa lugha ya Kiswahili kwa ushirikano na vyombo vya habari vya Tanzania ni pamoja na DW ya Ujerumani,VOA ya Marekani,BBC ya Uingereza.RFI ya Ufaransa,idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa mataifa.idhaa ya Kiswahili ya Redio China,Idhaa ya Kiswahili ya Redio Japan ambazo zote zinakwenda kuguswa moja kwa moja na mabadiliko haya ya kikanuni za maudhui ya Redio na Televisheni nchini Tanzania.
Chanzo: DW