1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tahadhari kuhusu uuzaji wa dawa za kughushi nchini Kenya

Wakio Mbogho31 Mei 2022

Baraza la magavana nchini Kenya limelalamika na kutoa tahadhari kuhusu uuzaji wa dawa za kughushi za kutibu saratani na wizi wa dawa kwenye hospitali za umma.

https://p.dw.com/p/4C5HB
Cancer Drugs False Claims Celgene
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Derer

Baraza la magavana nchini Kenya linaitaka wizara ya afya kuweka mikakati ya dharura kukomesha uuzaji wa dawa za kughushi na wizi wa dawa za kutibu saratani. Mwenyekiti wa kamati ya afya katika baraza hilo, gavana Peter Anyang' Nyong`o ameeleza.

"Kuna ripoti kwamba watu walioko kwenye wodi ya wagonjwa wa saratani na ya wagonjwa mahututi wamenyimwa dawa zao, na wakapewa dawa za kughushi, katika taifa hili la Kenya.”

Ripoti ya muungano wa mashirika yanayoangazia ugonjwa wa saratani nchini Kenya, imeuorodhesha ugonjwa wa saratani kama wa tatu kwenye sababu kuu za vifo nchini, ikionyesha kuwa visa 42,116 vipya huripotiwa kila mwaka, na vifo 27,092 hurekodiwa kila mwaka kutokana na saratani.

Soma pia→Mwamko wa wanawake kuhusu saratani ya kizazi ni mdogo

''Inakuwa vigumu sana kuutibu ugonjwa huo''

Catherine Wachira, mwenyekiti wa muungano huo, anasema wamepokea malalamiko ya wagonjwa wa saratani kukosa kupewa matibabu yanayofaa.

"Mifumo ya hospitali ya Kenyatta inapaswa kufanyiwa ukaguzi. Hapo ndipo wagonjwa wengi huenda, na wakati tunapokuwa na ukosefu wa dawa au vifaa vya kutibu saratani kuharibika, inatia wasiwasi sana kwa sababu wakati mgonjwa wa saratani anakosa matibabu yake, inakuwa vigumu sana kuutibu ugonjwa huo.”

Soma pia →Saratani yawakumba wengi Kenya

Visa vya wizi wa dawa za saratani hospitali ya Kenyatta

Wafanyakazi wa hospitali ya Kenyatta walishitakiwa kwa wizi wa dawa
Wafanyakazi wa hospitali ya Kenyatta walishitakiwa kwa wizi wa dawaPicha: Reuters/O.Sanadiki

Wiki iliyopita wafanyakazi sita wa hospitali kuu ya kitaifa ya rufaa ya Kenyatta walishtakiwa kwa wizi wa dawa za saratani zenye thamani ya shilingi milioni 4.6. Hospitali hiyo ambayo ni ya rufaa ni ya umma na hushughulikia idadi kubwa zaidi ya wagonjwa nchini Kenya, hasa wanaougua magonjwa sugu. Ilibainika kwamba dawa zilizoibwa zilipelekwa katika kliniki zinazomilikiwa na baadhi ya wafanyakazi wa hospitali kuu ya Kenyatta.

"Inaweza ikafanyika kwa ufanisi zaidi kwa kuhakikisha kwamba, usambazaji umenakiliwa kupitia njia ya kielektroniki. Ndiposa dawa zinapotoka kwenye kitengo cha kuhifadhia dawa na kupelekwa kwenye wodi ya hospitali, ni jambo ambalo linaweza kufuatiliwa bila makosa yoyote.”

Kwa wagonjwa wa saratani nchini, hili ni pigo kubwa. Tayari wengi wao hulazimika kusubiri kwa muda mrefu ili kupokea matibabu kwenye hospitali za umma, kutokana na orodha ndefu za wagonjwa, wataalam wachache na vifaa vichache.