Tafiti za saratani: Je dawa zilizopo zinatibu?
4 Februari 2021Mara zote mchakato wa kutengeneza dawa huchukua muda mrefu sana na mara nyingine hutoa matokeo yasiyotarajiwa kabisa, kama ilivyo kwa Aspirin na Viagra. Watafiti katika kipindi hiki wamekuwa wakitumia kanzidata ya dawa katika mchakato wa kuvumbua dawa mpya ya kukabiliana na viini vinavyosababisha saratani
Dawa hutengenezwa kwa malengo mahususi, kubwa likiwa ni kupunguza maumivu ama kushusha shinikizo la damu au labda kutibu ugonjwa fulani. Lakini hata hivyo, mchakato wa uzalishaji wake hukabiliwa na milima na mabonde. Kwa wastani huchukua hadi miaka 13 kwa dawa kuthibitishwa na pengine hata zisifikie hatua hiyo.
Licha ya hayo, mara nyingine huwa na matokeo mazuri na ya kushangaza na hasa inapotokea dawa inayotenegezwa kwa lengo fulani inapochanganywa na viungo vingine baadaye huleta matokeo tofauti na ambayo hayakutarajiwa.
Na watafiti wa saratani nao hivi sasa wamejikita katika njia hiyo ya kutengeneza dawa nyingine miongoni mwa zilizopo, wakati wakiendelea na tafiti za tiba ya saratani.
Faida ya njia hii ni kwamba mchakato huo mrefu wa utafiti na kuthibitishwa tayari unakuwa umekamilika, lakini pia viungo vingine muhimu vinakuwa tayari vimepatikana na kuthibitishwa kuwa salama kwa matumizi. Njia hiyo pia ni ya haraka na nafuu tofauti na ile inayotaka dawa mpya kuthibitishwa kwanza.
Soma Zaidi: WHO yazindua mikakati ya kupambana na Saratani ya kizazi
Mwaka 2020, watafiti kutoka taasisi ya saratani ya UT Southwestern Simmons waligundua mchanganyiko wa dawa ulioweza kuzuia ukuaji zaidi wa seli za saratani. Watafiti wa chuo kikuu cha Bergen huko Norway, kwa miaka kadhaa wamekuwa wakijaribisha mamia ya aina za dawa na namna zinavyoweza kupambana na seli za saratani. Wamegundua kwamba dawa zilizotumika kupambana na vimelea kama minyoo zina viungo vya nitazoxanide vilivyopo kwenye dawa zinazotumika kutibu saratani ya tezi dume na utumbo mkubwa.
Hata hivyo si wakati wote watafiti hugundua viungo katika dawa vinavyoweza kutibu maradhi mengine kwa kiwango cha juu hivyo kuhimiza tafiti zaidi, kama wanasayansi wa taasisi mbalimbali walivyochapisha uchunguzi wao katika jarida la masuala ya saratani la Nature Reviews Cancer ambalo ni kubwa kabisa na la aina yake.
Wao walitumia kanzidata ya zaidi ya aina 6,000 za dawa zilizokuwepo hadi mwaka 2020 ambazo ama zilikuwa zimethibitishwa na mamlaka ya dawa ya Marekani au zilizoonyesha usalama wakati wa majaribio.
Kwenye utafiti huo, waligundua takriban viungo 50 ambavyo havikugunduliwa bado kuwa vinaweza kukabiliana na saratani. Kwa msingi huo basi, kasi ya utengezwaji wa dawa mpya ya saratani inaweza ama kuongezeka au dawa zilizopo zinaweza kutumika lakini kwa namna nyingine.
Kulingana na mwandishi kiongozi wa uchunguzi huo Steven Corsello, ugunduzi mkubwa kabisa ulionyesha kiungo cha acetylsalicylic acid, ASA kilichopo kwenye Aspirin, dawa iliyotengenezwa kwa lengo la kupunguza maumivu, kinaweza kuzuia shambulizi la moyo na kiharusi.
Hata ugunduzi wa Viagra zinazotumika kuongeza nguvu za kiume pia ulikuwa kama bahati mbaya tu. Awali, kiungo kikubwa kabisa cha sildenafil kwenye dawa hiyo kilikuwa ni ajili ya kutibu maradhi ya moyo na shinikizo la damu.
Katika wakati huu ambao macho ya wanasayansi yamegeukia chanjo na tiba ya COVID-19, kila mmoja achukue hatua za kujilinda. Epuka matumizi ya tumbaku, fanya vipimo vya saratani, epuka kukaa kwenye jua kali, punguza uzito, tibu maradhi ya kuambukiza kama ya homa ya ini na bakteria wa HPylori na kubwa, epuka kunywa pombe.
Tizama Video:
Mashirika: DW