1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SURA YA UJERUMANI NA MIAKA 25 TANGU KUASISIWA CHAMA CHA KIJANI-WALINZI WA USAFI WA MAZINGIRA:

14 Januari 2005
https://p.dw.com/p/CHhn

SURA YA UJERUMANI:

Chama cha KIJANI cha Ujerumani –chama cha walinzi wa usafi wa mazingira,kimeadhimisha wiki hii miaka 25 tangu kuasisiwa ,Januari 13, 1980.

Wakati ule kilionekana kama ‘hatari kwa demokrasia’ nchini Ujerumani na hivyo ndivyo Kiongozi mashuhuri wa chama-tawala cha Social Democratic Party Egon Bahr alivyokieleza chama hicho enzi zile.

Chama cha KIJANI-GREEN- kiliibuka kama mkusanyiko wa juhudi za raia mbali mbali kutoka vikundi mbali mbali vilivyokerwa na uchafuzi wa mazingira,vilivyojitolea kupigania amani na kupinga vita pamoja na vinu vya umeme vya kinuklia.

Miaka 3 baadae hapo Januari 13,1980 vikundi hivyo tofauti vya wakereketwa wa mazingira vikajumuika pamoja na kukiasisi chama hiki.Leo chama cha KIJANi kinatawala pamoja na chama cha kijamaa cha SPD cha Kanzela Gerhard Schröder.

Sura ya Ujerumani leo basi inaikagua miaka 25 ya chama hiki ambacho kimetoa waziri wa sasa wa mambo ya nje wa Ujerumani, Joshka Fischer.

Chama cha walinzi wa mazingira –KIJANI au GRÜNEN- kama kinavyojulikana nyumbani, kiliasisiwa januari 13, 1980 na mbali na kuwa kimeunda serikali ya muungano ya ujerumani pamoja na chama cha SPD mjini Berlin,kinawakilishwa pia katika sehemu kubwa ya mabunge ya mikoa.

Kwa ufupi kinyume na vyama vyengine vilivyoibuka miaka ya karibuni ,chama cha wakereketwa wa mazingira cha KIJANI kimekubalika hii leo na sehemu ya jamii ya wapigakura wa Ujerumani kama matokeo kadhaa ya chaguzi za serikali za mabaraza ya miji,mikoa na bunge la shirikisho yalivyobainisha.

Lakini mwanzo haukua rahisi hivyo:kwani mara tu baada ya kuasisiwa chama hiki Januari,1980 mjini Karlsruhe, wachambuzi wengine wa habari walikwishakata hatima ya chama hiki-yaani hakitadumu:Vichwa vya habari kama hivi viliibuka: "MWISHO WA MATUMAINI YA KIJANI"-hilo lilikua gazeti la Süddeutsche Zeitung.

"Wazushaji fujo wanazama."-Jarida la Spiegel.

Vichwa hivyo vya habari lakini, vilikua na chanzo chake :Wakereketwa hawa walikorofishana hasa juu ya mada ya kuwakubali kuwa wanachama wafuasi wa siasa kali za mrengo wa shoto na mada hii ilikua ya mvutano mkubwa na wa muda mrefu.Yaliibuka mabawa 2 chamani –bawa la wenye siasa kali za kimazingira-waliotwa Fundis walioshikilia kikakamavu nadharia kali za kimazingira na wale waliochukua msimamo wa wastani unaotambua hali ya ukweli wa mambo ulivyo nchini ‘REALOS".

Lakini hata katika jukwaa lao la siasa,chama cha KIJANI tangu mwazo wakuwa na pipa la baruti .Kwa madai yao ya kuvifunga vinu vyote vya nguvu za nuklia vinavyozalisha umeme nchini, kuvunjwa kwa Shirika la Ulinzi la Magharibi-NATO na kurekebisha uchumi na viwanda vya nchi hii kufuata mfumo wa kimazingira na sio kuchafua viwanda mazingira.

Msisitizo wa mada hii uliwekwa katika kile kilichoitwa ‘UMWELTSCHUTZ"-ulinzi wa mazingira yetu na katika mada hii chama cha KIJANI kimefanikiwa mno mnamo miaka hii 25 kuizindua jamii ya wajerumani na hata nchi jirani haja ya kulinda usafi wa mazimngira yetu.

Mtaalamu wa fani ya vyama vya kisiasa wa kijerumani KARL-RUDOLF KORTE anaefunza katika Chuo Kikuu cha DUISBURG na ESSEN anasema:

"Hali hiyo imeongoza mada za usafi wa mazingira kujumuishwa katika jukwaa na mipango ya vyama vyengine mashuhuri vilivyotia mizizi nchini.hii ikaongoza zaidi kuazishwa wizara za ulinzi wa mazingira,na hii ikawa awamu ya kwanza ya mafanikio kwa chama cha KIJANI.

Kwani vyama vyengine vimefuata nyayo zachama cha KIJANI na wakati huo huo lakini chama hicho kimebanwa kujitanua katika uwanja wa mazingira katika kipindi hiki."-

Isitoshe, chama hiki kikawekewa mipaka zaidi ya kujitanua kutokana na jukwaa lake binafsi la kisiasa. Kilianzisha utaratibu wa zamu miongoni mwa wabunge wake.Ikiwa kipindi cha mbunge kuwa Bungeni ni miaka 4, mmoja atawakilisha chama na wilaya yake kwa miaka 2 halafu atampisha mwengine pia atumike kwa miaka 2.Pia kilianzisha mfumo mkali ulioselelea hadi karibuni wa kutenganisha madaraka Bungeni na yale chamani.

Kutokana na kiu kikubwa katika jamii cha na njia nyengine ya kutunza mazingira kuliko iliokuwapo,chama cha walinzi wa mazingira kikawa kinajipatia kura na mafanikio makubwa kutoka uchaguzi mmoja hadi mwengine.Mafanikio makubwa katika kipindi hiki,yakawa kuundwa kwa serikali ya kwanza ya muungano kati ya chama cha kijamaa cha SPD na cha KIJANI katika mkoa wa Hesse, hapo 1985.

Aliesadifu wakati ule kuwa waziri wa kwanza wa ulinzi wa mazingira katika serikali hiyo ni Joshka Fischer,leo waziri wa nje wa Ujerumani.

Lakini ingawa chama cha KIJANI kikimurika ufanisi kutoka nje, ndani lakini mizozano ilikua haishi na takriba kila mwaka zikiibuka sura mpya katika uongozi wake .Mivutano kati ya wafuasi wake wenye siasa kakamavu za mrengo wa shoto kabisa-FUNDIS na wale wa siasa wastani ‘REALOS" wakipeana changamoto kuhusu mustakbala wa chama.

Matokeo yake mabaya kabisa ya mvutano huu yakadhihirika 1990 pale nchi 2 za Ujerumani zilipoungana tena:

Katika uchaguzi wa mwaka huo,Chama cha KIJANi cha Ujerumani Magharibi wakati ule, kilishindwa hata kujipatia 5% ya kura kuweza kuwakilishwa Bungeni.Kwani kilikosea biramu lake la uchaguzi kilipodai:WOTE WANASZUNGUMZIA UJERUMANI.SISI TUNAZUNGUMZIA MAZINGIRA’.Biramu hilo katika kipindi cha hamasa na hisia za uzalendo wa kuungana tena kwa wajerumani tangu vita vya pili vya dunia, hazikukisaidia chama cha KIJANI na biramu lao la mazingira.Ikawa damu nzito kuliko maji.

Ilichukua hadi 1993, ndipo matawi 2 ya vyama vya KIJANI vya ulinzi wa mazingira-moja la magharibi na jengine la Mashariki-kuungana na kuunda BUNDNIS 90/DIE GRÜNEN na kuwa nguvu moja ya walinzi wa mazingira.

1994 muungano huu ukaweza kuwarudisha walinzi wa mazingira Bungeni na hasa kutokana na sera za wastani za waziri wa sasa wa mambo ya nje Joshka Fischer,anaeelemea lile bawa la Realos-bawa la wafuasi wa siasa za wastani kulingana na ukweli wa hali ya mambo ilivyo.

Kwa mchango wa Bw.Fischer ambae alikiongoza kikundi cha wabunge wa chama Bungeni,chama cha KIJANI kikaweza miaka 4 baadae kubalighi kweli kisiasa:1998 kiliunda pamoja na chama cha SPD cha Kanzela Schröder serikali ya Shirikisho mjini Berlin.

Jinsi sera za chama hiki zilivyogeuka kinyume na awali kiliponadi vita kwa shirika la kijeshi la NATO na kutaka livunjwe,chama cha KIJANI kimeidhinisha kujiingiza kijeshi kwa NATO katika mgogoro wa KOSOVO na hii ilitokana tu na juhudi za Bw.Joshka Fischer kama asemavyo mtaalamu wa sura ya vya vya kisiasa hapa Ujerumani Korte:

"Swali hilo lilikuwa nyeti kabisa.Kwamba Bw.Fischer alifaulu kubadili msimamo huo sifa zafaa ni zake.Kutka chama kilichokua kikipinga vita chama kinachotetea amani ,kubadili msimamo ulikua mtihani mkubwa.Iliwezekana lakini sio bila ya mvutano,lakini imewezekana."

Pamoja na chama cha SPD chama cha KIJANI kimepitisha maazimio kadhaa magumu miaka iliofuatia:mageuzi ya mfumo wa malipo ya kodi na jamii,hatua zaidi za kutumika kwa wanajeshi wa Ujerumani kuhifadhi amani nchi za nje kama vile Mazedonia na Afghanistan ziliidhinishwa na kupitishwa.

Kwahivyo, wakati chama cha SPD kilishinda chupuchupu tu uchaguzi wa 2002 na katika chaguzi zilizofuatia kikipoteza kura kila kukicha,chama cha KJANI kimekuwa kikitia fora na kudhibiti nguvu zake pale pale.

Kwa mtaalamu Korte,hii haistaajabishi na anaona chama hiki hakitasalia daima mshirika wa kuunda serikali ya muungano na chama cha SPD pekee bali hata na vyama vyengine.Katika mabaraza ya miji tayari hii imeshatokea, mfano katika mkoa huu wa Northrhein Westphalia.Huko chama cha KIJANI kimeunda serikali nyingi zaidi za muungano na chama cha Upinzani cha CDU kuliko SPD.Na ingelikua anasema mtaalamu korte uchaguzi ujao katika mkoa wa Baden-Würtemberg hauko karibu sana na ule wa mwakani wa shirikisho,pengine serikali ya muungano kati ya CDU na KIJANI ingeliundwa katika daraja ya kimkoa.,"