Sudan yasusia mazungumzo ya amani nchini Ethiopia
11 Julai 2023Jumuiya ya nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD, iliwaalika pande mbili hasimu kwenye mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Ethiopia jana, wakati mapigano yakiendelea kote nchini Sudan. Burhan na Daglo hawakuhudhuria moja kwa moja mazungumzo hayo mjini Addis Ababa, ingawa kundi la RSF lilituma mwakilishi kwenye mkutano huo ulioongozwa na Kenya, Sudan Kusini, Djibouti na Ethiopia.
Wizara ya mambo ya nje ya Sudan imesema katika taarifa kuwa ujumbe wake hautashiriki hadi ombi lake la kuiondoa Kenya kama mwenyekiti wa mazungumzo hayo litimizwe, huku wakiomba rais wa Kenya William Ruto abadilishwe haswa kwa sababu ya kile walichokiita upendeleo wake.
Wizara ya Mambo ya nje ya Kenya na Ofisi ya Ruto hawakujibu mara moja juu ya kauli hiyo lakini Serikali ya Kenya ilisema mwezi uliopita kuwa rais Ruto hakuwa na upande wowote anaoegemea katika mzozo huo na kwamba ni msuluhishi ambaye aliteuliwa ipasavyo na mkutano wa kilele wa IGAD.
Soma pia: Umoja wa Mataifa: Sudan ipo hatarini kuingia 'vita kamili'
Kufuatia mkutano huo, Ruto ametoa wito wa kutekeleza bila masharti mpango wa usitishaji mapigano na kuanzishwa kwa eneo salama karibu kilomita 30 viungani mwa mji mkuu Khartoum ili kufanikisha zoezi la utoaji wa misaada ya kibinadamu. Wito kama huo umetolewa pia na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed:
" Pande zote katika mzozo huu wenye ghasia zitalazimika kusitisha mtutu wa bunduki na kuafiki mara moja na bila masharti mpango wa kudumu wa usitishaji mapigano."
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), Martin Griffiths ameibua tatizo la kukosekana kwa njia salama ya kuwasilisha misaada:
" Sudan huenda ni sehemu tete zaidi duniani kwa sasa linapokuja suala la kuwasilisha misaada ya kibinadamu, na tatizo hili linajitokeza kwa sababu ya kukosekana kwa njia bora na salama katika maeneo yanayotakiwa kuepushwa na vita."
Mikutano mbalimbali kuhusu mzozo wa Sudan
IGAD imesema katika taarifa yake kuwa imeafiki kutoa wito wa kufanyika mkutano wa kilele wa chombo kingine cha kikanda ambacho ni Baraza la Kudumu la Afrika Mashariki ili kutafakari namna ya kupeleka wanajeshi wa kikosi cha EASF ili kulinda raia baada ya karibu miezi mitatu ya mapigano kati ya Jeshi na vikosi vya RSF. Sudan ni mwanachama wa vyombo vyote viwili, kama ilivyo kwa Ethiopia, Kenya, Somalia na Uganda.
Soma pia: Guterres alaani shambulio la anga lililowaua watu 22 Sudan
Juhudi za kidiplomasia za kujaribu kuumaliza mzozo huo hadi sasa zimeambulia patupu huku kukiwa na harakati mbalimbali zinazokinzana na zinazoleta mkanganyiko wa jinsi pande zinazozozana zinavyoweza kuletwa kwenye meza ya mazungumzo. Hata hivyo IGAD imetaja kusikitishwa na kitendo cha wajumbe jeshi la Sudan kususia mazungumzo hayo licha ya kuthibitisha hapo awali kuwa wangehudhuria.
Mazungumzo yaliyoandaliwa mjini Jeddah na kufadhiliwa na Marekani pamoja na Saudi Arabia yalisitishwa mwezi uliopita. Misri hata hivyo imesema itakuwa mwenyeji wa mkutano mwingine wa kilele wa majirani wa Sudan ifikapo Julai 13 ili nao pia wajadili namna ya kuumaliza mzozo huo.