1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia yakubaliana kuhusu uchaguzi

Kyama28 Mei 2021

Jumuiya ya kimataifa imekaribisha hatua ya viongozi wa kisiasa nchini Somalia ya kufikia makubaliano kuhusu mfumo wa kuendesha uchaguzi uliocheleweshwa.

https://p.dw.com/p/3u6KA

Kulingana na makubaliano hayo yaliyosainiwa jana Alhamisi na Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble na wawakilishi wa majimbo matano, sasa huenda mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu nchini humo ukaanza, na uchaguzi kufanyika hatimaye katika kipindi cha siku 60. 

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia,  James Swan amesifu juhudi za serikali ya shirikisho na viongozi wa majimbo na pia makundi mbalimbali nchini humo kwa kufikia makubaliano ya pamoja kwa lengo la kukomesha mkorogano wa kisiasa na kuleta mustakabali mpya wa nchi hiyo ya pembe ya Afrika iliyoathirika vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe. 

"Kwa mara nyingine tena ningependa kuwasihi viongozi wa Somalia kutafuta suluhu kwa njia ya maridhiano na kuonyesha uongozi mwema na wa busara unaohitajika wakati wa kipindi hiki muhimu cha kihistoria. [Viongozi] waliotia saini mkataba wa Septemba 17 ni sharti wafanye maamuzi kamili kuhusu hatima ya nchi hiyo kwa kuandaa uchaguzi." amesema Mwanadiplomasia huyo.

Abdirizak: Uchaguzi utakuwa huru na wa haki 

Somalia Mogadischu Selbstmordanschlag Polizei
Kuchelewashwa uchaguzi kumekuwa chanzo cha mvutano Somalia Picha: Sadak Mohamed/AA/picture alliance

Naye Waziri wa mashauri ya kigeni wa Somalia Mohamed Abdirizak ameliahidi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa serikali ya mjini Mogadishu imefikia makubaliano na tawala za majimbo ili hatimaye kuwezesha uchaguzi wa kitaifa uliocheleweshwa kufanyika.

"Kwa sasa tumefikia makubaliano ambayo yatawezesha Somalia kuwa na uchaguzi huru na wa haki. Tokea sasa, Somalia itahitaji kuwa na utawala wa kisiasa wa mpito unaozingatia uchaguzi huru na wa haki. Lakini hiyo ni changamoto kubwa na itahitaji mshikamano kutoka kwa jamii ya Wasomali, serikali na washirika wake kwa jumla kwa minajili ya kuleta amani na maendeleo nchini humo." amekaririwa afisa huyo wa serikali

Hivi karibuni duru zimearifu kuwa kufuatia makubaliano hayo yaliyofikiwa jana Alhamisi mjini Mogadishu, mchakato wa uchaguzi unatarajiwa kuandaliwa katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

Tarehe kamili ya uchaguzi itapangwa 

Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed
Rais wa Somalia Mohamed Farmajo Picha: Vladimir Smirnov/TASS/imago images

Tarehe kamili ya uchaguzi wa rais na bunge itaamuliwa na bodi ya uchaguzi na mchakato mzima utasimamiwa na afisi ya waziri mkuu, Mohamed Hussein Roble.

Hali ya kisiasa nchini Somalia, imekuwa katika njia panda tangu kutibuka kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Februari kutokana na mkorogano baina ya makundi ya kisiasa nchini humo.


Umoja wa Mataifa umekuwa ukimshinikiza Rais Mohamed Abdullahi “Farmajo” kuitisha mazungumzo kati ya serikali yake na tawala za majimbo ili kukubaliana juu ya utaratibu wa kuandaa uchaguzi mkuu haraka iwezekanavyo.