1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia ndio nchi hatari kabisa duniani

13 Julai 2011

Umoja wa Mataifa umesema Somalia ni eneo lenye janga kubwa kabisa la kibinaadamu hivi sasa duniani, huku vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vikiongezeka kwa sababu ya utapiamlo na ukosefu wa usalama.

https://p.dw.com/p/11tu5
Kamishna wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres

Wakimbizi wa Kisomali wanaokimbia ukame na njaa kwao na kutafuta hifadhi nchini Kenya, wanatajwa kuwa ndio watu mafukara wa mwisho na watu walio kwenye hatari kubwa kabisa duniani.

Hayo ni kwa mujibu wa Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Antonio Guterres, ambaye ametembelea kambi ya Dadaab nchini Kenya, kujionea mwenyewe hali halisi ya janga hilo.

Guterres amesema idadi ya watoto wanaokufa kutokana na ukosefu wa lishe inaongezeka, baada ya kusubiri kwa wiki kadhaa kupokea msaada wa dharura bila mafanikio.

"Sina shaka kwamba leo Somalia ni janga kubwa kabisa la kibinaadamu tunalokabiliana nalo ulimwenguni. Nimetembelea kambi nyingi sana za wakimbizi duniani, lakini hapa Dadaab tuna watu ambao ni masikini wa masikini, walioko hatarini ya walio hatarini duniani." Amesema Guterres.

Mmoja wa wakimbizi hao, Ulmay Abdou Ishaq, amesema wanakimbia Somalia kwa sababu ya njaa. "Hatuna kitu cha kula wala kunywa tukiwa safarini."

Wakimbizi katika kambi ya Dagahaley katika eneo la Dadaab, Kenya.
Wakimbizi katika kambi ya Dagahaley katika eneo la Dadaab, Kenya.Picha: Picture-Alliance/dpa

Ulmay ametumia wiki tatu akitembea kutoka Somalia kuelekea kambi ya Dadaab, nchini Kenya akiwa na watoto wake sita na mume wake ambaye ni mgonjwa.

Mkimbizi mwengine, Muslima Adan Hassan, mwenye miaka 35, alifiliwa na watoto wake wawili wa kiume na mmoja wa kike katika siku zao 35 za kupigania kufika kwenye kambi ya Dadaab, nchini Kenya.

Kutoka mpakani mwa Somalia na Kenya hadi kwenye kambi ya Dadaab, wakimbizi hupaswa kutembea kwa miguu umbali wa kilomita 80 kupitia jangwani.

Mkimbizi mmoja, Abdullahi Hussein Sheikh, amesema kwamba kumekuwepo na visa vya watoto kuliwa na wanyama wakali kama vile simba na fisi.

Mwezi uliopita, idadi ya wakimbizi wapya kwenye kambi ya Dadaab ilifikia 1,300 kwa siku, likiwa ni ongezeko la mara tatu. Mashirika ya misaada yanashindwa kutoa misaada ndani ya Somalia, kutokana na ukosefu wa usalama na uadui kutoka kundi la Al-Shabbaab, linalodhibiti sehemu kubwa ya nchi.

Ukame kwenye kambi ya Dagahaley, Kenya
Ukame kwenye kambi ya Dagahaley, KenyaPicha: dapd

Taswira kwenye kambi ya Dadaab kwenyewe ni ya kutisha sana, huku ikielezwa kwamba watoto na mama zao wanaonekana wanagaragara kwenye mchanga kutokana na kuishiwa nguvu kwa njaa. Wengi wao hawamiliki chochote zaidi ya mageleni ya maji na nyuso zilizopauka kwa vumbi.

Idadi ya watoto wanaofariki chini ya miaka mitano imeongezeka mara sita tangu mwaka jana katika eneo la Dagahaley, ambayo ni sehemu ya kaskazini ya kambi ya Dadaab. Kiasi ya asilimia 24 ya watoto wanaowasili kambini hapo, tayari wana utapiamlo.

Mtaalamu wa lishe wa Shirika la UNHCR, Allison Oman amesema kwamba wengi kati ya watoto hao, hufariki dunia masaa 24 baada ya kuwasili kwao.

Umoja wa Mataifa umeuelezea ukame unaolikumba sasa eneo la Pembe ya Afrika kwamba haujawahi kutokea kwa miaka 60 iliyopita. Umoja huo umeutangaza ukame huu kuwa hali ya dharura, ambayo ni hatua moja tu kabla ya kutangazwa rasmi kuwa baa la njaa. Kiasi ya watu milioni 10 katika nchi za Kenya, Somalia na Ethiopia wanakabiliwa na tatizo hili.

Somalia imekuwa haina serikali imara kwa miongo miwili sasa, jambo ambalo linaongeza athari za kukabiliana na ukame. Wanamgambo wa Al-Shabbaab wamekataa kuyaruhusu mashirika ya misaada kugawa chakula katika maeneo wanayoyadhibiti, wakidai kuwa jambo hilo linachochea utegemezi.

Hata hivyo, wiki iliyopita wanamgambo hao walibadilisha msimamo wao na kutangaza kwamba mashirika ya misaada ya kibinaadamu yanakaribishwa nchini Somalia, lakini tangazo hili limepokelewa kwa tahadhari.

Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema kwamba ni lazima sera hii mpya ya Al-Shabbaab ijaribiwe na ithibitishwe kama inaweza kuzuia mateso ya watu na kuwafanya wasikimbie nchi yao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Oummilkheir Hamidou