1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silvio Berlusconi: Mwisho wa enzi?

3 Oktoba 2013

Akiwa ametelekezwa na wasaidizi wake, huku akiandamwa na kesi za kisheria, kushindwa kwa Silvio Berlusconi na waziri mkuu wa Italia, Enrico Letta, kunaelezwa kuwa miwsho wake kisiasa.

https://p.dw.com/p/19tNe
Waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi.
Waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi.Picha: Reuters

"Nadhani tunashuhudia ukurasa wa mwisho katika maisha ya kisiasa ya Berlusconi," alisema Giacomo Marramao, Profesa katika Chuo Kikuu cha Tre cha mjini Roma, baada ya kumalizika kwa kura ya imani kwa serikali katika bunge la Italia. Marramao alisema matokeo ya kura hiyo yaliashiria kupungua kwa kuaminika, akielezea mgawiko miongoni mwa wabunge wa chama cha Berlusconi cha People of Freedom PDL. Profesa huyo alisema chama cha baada ya Berlusconi kimezaliwa siku hiyo ya Jumatano.

Baada ya miongo miwili katika siasa, tajiri huyo machachari ambaye aliwahi kujilinganisha na Yesu, alionekana kubaki mpweke, baada ya makada wake kuanza kumtupa mkono mmoja baada ya mwingine, na kuiunga mkono serikali. Wakati Berlusconi anaondoka bungeni, baada ya kubadili ghafla msimamo wake wa kuiangusha serikali ya waziri mkuu Letta, na kuunga mkono kura ya imani, kundi la waandamanaji lilikuwa nje likimzomea na kumuambia, "Toka hapa."

Waziri mkuu wa sasa wa Italia, Enrico Letta.
Waziri mkuu wa sasa wa Italia, Enrico Letta.Picha: picture-alliance/dpa

Katika kivuli cha Berlusconi halisi
Hata kabla ya kubadili msimamo wake, wachambuzi walisema taarifa zake za kuchanganya zilikuwa zinaonyesha mtu aliyeishiwa nguvu. Stefano Folli, mwandishi wa makala katika gazeti la biashara la kila siku la II Sole 24 Ore alisema Berlusconi alionekana kama kivuli cha Berlusconi wa zamani. Filippo Ceccarelli, mwandishi wa gazeti linaloegemea mrengo wa shoto la La Repubblica, yeye alikwenda mbali na kuilinganisha kura ya Jumatano na Julai 25 mwaka 1943, wakati alipoangushwa rasmi dikteta Benito Mussolini katika kura na baraza kuu la Kifashisti. "Dunia nzima inaanguka," alisema Ceccarelli.

Kitisho halisi kwa Berlusconi hata hivyo, hakitokani na kudhalilishwa kwake bungeni, ambako amefanikiwa kurudi hapo kabla, lakini katika masaibu yake ya kisheria yanayozidi, walisema wachambuzi. James Walston, Profesa wa ushirikiano wa kimataifa katika chuo kikuu cha Marekani mjini Roma, alisema Berlusconi hana tena udhibiti kamili wa chama chake, lakini bado ana nguvu. Lakini aliongeza kuwa masaibu yake ya kisheria yanayoongezeka kila kukicha, yanaashiria kuondoka kwake muda wowote.

Mlolongo wa kesi dhidi yake
Berlusconi anatarajiwa kufukuzwa bungeni mwezi huu, na kuzuwiwa kugombea katika uchaguzi ujao, baada ya kukutikana na hatia katika kesi ya udanganyifu wa kodi mwezi Agosti. Na jaji mjini Milan ataamua mwezi huu, iwapo hukumu ya kifungo cha miezi 12 aliyopewa aitumikie katika kifungo cha nyumbani au afanye kazi za kijamii - hatma ya kufedhehesha kwa bilionea huyo aliyekuwa na nguvu kubwa.

Mambo bado! Ushawishi wa Berlusconi katika siasa za Italia waanza kuyeyuka.
Mambo bado! Ushawishi wa Berlusconi katika siasa za Italia waanza kuyeyuka.Picha: picture alliance/ROPI

Berlusconi mwenye umri wa miaka 77 pia alikataa rufaa dhidi ya kifungo cha miaka saba jela, alichohukumiwa kwa kufanya ngono na changudoa aliekuwa chini ya umri, na kwa matumizi mabaya ya ofisi alipokuwa waziri mkuu, na vile vile hukumu nyingine ya kifungo cha mwaka moja jela kwa kuvujisha siri za polisi kwa lengo la kumchafua mpinzani wake.

Ishara ya kuanguka kwa Berlusconi ilionyeshwa katika picha zilizosambazwa mapema wiki hii, zikimuonyesha akiwa amebeba mbwa wake katika makaazi yake, katika kile gazeti la La Repubblica lilichosema ni kutokana na ukweli kwamba, mbwa huyo ndiyo kiumbe pekee ambaye kiongozi huyo alieko katika kingo za kuporomoka, anaweza kumuamini.

Lakini Berlusconi amefanikiwa kurudi ulingoni huko nyuma, ingawa hakuwa katika hali ya udhaifu aliyomo hivi sasa, na baadhi ya wachambuzi wameondoa uwezekano wa yeye kutoka katika hili.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo.