1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Italia yashinda kura ya imani

Admin.WagnerD2 Oktoba 2013

Waziri mkuu wa Italia Enrico Letta amepata ushindi katika kura ya imani kwa serikali yake, baada ya waziri mkuu wa zamani Silvio Berlusconi kubadilisha mipango yake ya kuuangusha muungano unaotawala nchini humo.

https://p.dw.com/p/19szH
Waziri Mkuu wa Italia Enrico Letta, amevuka kiunzi cha kura ya imani bungeni
Waziri Mkuu wa Italia Enrico Letta, amevuka kiunzi cha kura ya imani bungeniPicha: Reuters/Heinz-Peter Bader

Letta amepata kura 235 katika baraza la juu ya bunge la Italia- Seneti, ambako alikuwa katika hatari ya kukosa wingi unaohitajika wa kura 161 kwa kura 20, iwapo mpango wa Berlusconi kujiengua ungetimia. Maseneta 70 walipiga kura ya kumpinga. Akizungumza katika bunge hilo lililojaa hamasa, Berlusconi alisema wameamua bila kinyongo kupiga kura ya kuwa na imani na serikali. Akifafanua uamuzi wake, Berlusconi alisema Italia inahitaji serikali ambayo inaweza kufanya mageuzi ya kimuundo na kitaasisi, ambayo nchi hiyo inayahitaji ili kuwa ya kisasa.

Luigi Zanda, ambaye alizungumza kwa niaba ya chama cha siasa za wastani za mrengo wa shoto cha Demokratik, PD alisema waziri mkuu huyo wa zamani alikuwa anajaribu kuficha pigo la kisiasa, ambalo hata hivyo liko wazi machoni mwa Wataliana. Kabla ya hotuba ya Berlusconi, kulikuwepo na taarifa kuwa 25 kati ya wabunge 91 kutoka chama chake cha kihafidhina cha People of Freedom PDL walikuwa tayari kupiga kura ya kuwa na imani na serikali.

Ufa katika chama cha Berlusconi

Chama cha PDL kiliendelea kuparaganyika licha ya kubadilisha msimamo katika dakika za mwisho wakati Francesco Nitto Palma, waziri wa zamani wa Sheria, alipotoka nje kuepuka kumuunga mkono Letta, na kufuatiwa na maseneta wengine wa chama hicho. Maseneta walioasi msimamo wa chama chao cha PDL waliongozwa na naibu kiongozi wa chama hicho ambaye pia ni naibu waziri mkuu Angelino Alfano, na waziri wa miundombinu Maurizio Lupi, ambaye anahusiana na vuguvugu la kihafidhina la kikatoliki lenye ushawishi mkubwa la Communion and Liberation.

Waziri Mkuu wa zamani Silvio Berlusconi alilazimika shingo upande kubadili msimamo
Waziri Mkuu wa zamani Silvio Berlusconi alilazimika shingo upande kubadili msimamoPicha: Reuters

Maafisa wa chama kinachoongoza muungano huo cha PD walisisitiza kuwa serikali haitaendelea kutegemea uungwaji mkono usioaminika wa waziri mkuu huyo wa zamani. Stefano Fassina, waziri mdogo kutoka chama cha PD, alisema Silvio Berlusconi ameshindwa vibaya, na kuanzia leo, hana umuhimu wowote wa kisiasa.

Masoko yanemeeka

Masoko ya hisa ya Italia yamepokea vyema matokeo ya kura hii, ambapo faharasi kuu katika soko la hisa la Milani, ilipanda kwa asilimia 0.65 kufikia saa tisa alasiri, wakati kiashirio muhimu cha hatari kilikuwa chini. Katika hotuba yake kabla ya kura hiyo, waziri mkuu Letta alisisitiza kuwa nchi hiyo inahitaji utulivu wa kisiasa ili kutoka katika mdororo wa muda mrefu wa kiuchumi na kuendeleza imani ya masoko.

Waziri mkuu huyo alisema anataka aendelee kuiongoza Italia hadi angalau mwishoni mwa mwaka ujao wa 2014, wakati Italia itakapokamilisha kipindi chake cha miezi sita ya urais wa mzunguko wa Umoja wa Ulaya. Berluscon alisema wiki iliyopita kuwa anajiondoa katika muungano wa serikali, baada washirika kukataa kuzuwia mchakato wa kumfukuza bungeni kutokana na kutiwa hatiani kwa kosa la kukwepa kodi. Atatumikia kifungo cha mwaka mmoja nyumbani au kufanya kazi za kijamii.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe, ape

Mhariri: Saum Yusuf